Deni la serikali ya Namibia limeongezeka kwa asilimia 10
Katika ripoti yake ya karibuni kabisa, Benki Kuu ya Namibia imetangaza kwamba, deni la serikali ya nchi hiyo limepanda na kufikia dola bilioni 164 za Namibia (kama dola bilioni 8.8 za Kimarekani) mwishoni mwa Desemba 2024 suala ambalo linaashiria ongezeko la asilimia 10.2 la deni hilo tangu mwanzoni mwa mwaka wa fedha wa 2024/25.
Taarifa ya karibuni zaidi ya Benki Kuu ya Namibia iliyotolewa kuhusu matukio ya robo mwaka imesema kwamba ongezeko hilo lilichangiwa na ukopaji wa ndani kupitia hazina na dhamana, wakati deni la nje pia lilipanda kutokana na kushuka kwa thamani ya sarafu ya nchi hiyo.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, deni la ndani la serikali ya Namibia lilikuwa linaongezeka kwa asilimia 13.1 mwaka hadi mwaka na kufikia dola bilioni 126.1 za Namibia, ikiwa ni asilimia 50.2 ya pato la taifa (GDP).
Deni la nje lilipanda kwa asilimia 1.5 hadi dola bilioni 37.9 za Namibia, hasa kutokana na kudhoofika sarafu ya dola ya Namibia, na kuongeza kuwa, jumla ya deni la serikali kama sehemu ya Pato la Taifa lilifikia asilimia 65.3 kutoka asilimia 63.9 mwaka uliopita.
Mikopo ya mataifa mbalimbali imeendelea kuwa sehemu kubwa zaidi ya deni la nje la Namibia, likichukua asilimia 46.1 licha ya kwamba kunaonekana kupungua deni hilo ikilinganishwa na mwaka uliopita.
Ili kudhibiti ukopaji, Namibia imejitolea kujumuisha fedha, ikiwa ni pamoja na kupunguza matumizi yasiyo ya lazima, kuboresha ukusanyaji wa mapato, na kuweka kipaumbele cha mikopo ya masharti nafuu kuliko kukopa kibiashara ili kupunguza gharama za kulipia madeni.