Mali: Muungano wa Mataifa ya Sahel umevuruga nguvu za ukoloni
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i124750-mali_muungano_wa_mataifa_ya_sahel_umevuruga_nguvu_za_ukoloni
Waziri wa Mambo ya Nje wa Mali, Abdoulaye Diop, amesema kuwa Muungano wa Mataifa ya Sahel (AES) ulioundwa na Mali, Niger na Burkina Faso mwaka 2023, umebadili kabisa mlingano wa nguvu za kimkakati kwa madola ya kikoloni ambayo yanataka kuendelea kutawala nchi hizo.
(last modified 2025-04-04T10:11:31+00:00 )
Apr 04, 2025 10:11 UTC
  • Mali: Muungano wa Mataifa ya Sahel umevuruga nguvu za ukoloni

Waziri wa Mambo ya Nje wa Mali, Abdoulaye Diop, amesema kuwa Muungano wa Mataifa ya Sahel (AES) ulioundwa na Mali, Niger na Burkina Faso mwaka 2023, umebadili kabisa mlingano wa nguvu za kimkakati kwa madola ya kikoloni ambayo yanataka kuendelea kutawala nchi hizo.

Diop amesema, "Hakika kuna changamoto kubwa…zinazotokana na nguvu za zamani za kikoloni au mataifa ya Magharibi, na pia kutoka kwa wahusika wa kikanda wanaotaka kutawala au kuongoza mataifa yetu."

Akizungumza Alhamisi mjini Moscow akiwa pamoja na mawaziri wenzake wa mambo ya nje kutoka Russia, Niger, na Burkina Faso, yaani Sergey Lavrov, Yaou Sangare Bakary, na Karamoko Jean-Marie Traore, Diop alikumbusha kuwa Urusi ndiyo nchi ya kwanza kutambua rasmi Muungano huo wa AES, na kuwa wanaelewana kwa pamoja kuhusu vita dhidi ya ugaidi na changamoto za usalama katika eneo la Sahel.

Aidha amesema: "Napenda kukumbusha dhamira yetu ya pamoja ya kuongeza juhudi za kupambana na ugaidi…pamoja na wale wanaofadhili ugaidi, kama vile Ukraine."

Aidha, Diop amesema  kuwa hivi sasa Russia si tu mshirika, bali ni "rafiki wa kweli" wa mataifa ya Sahel.

Muungano wa Mataifa ya Sahel (AES) ulianzishwa rasmi mwezi Septemba 2023, ikiwa ni ushirikiano wa mataifa matatu ya Afrika Magharibi yaliyo chini ya serikali za kijeshi ambazo ziliingia madarakani chini ya uungaji mkono mkubwa wa wananchi. Muungano huo  unelanga kuimarisha ushirikiano wa kisiasa, kiuchumi na kiusalama.

Kwa sasa, Muungano huo unafanya mabadiliko makubwa ya kistratejia ya kimataifa, ikiwemo kujiondoa kutoka Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi (ECOWAS) na Shirika la Kimataifa la La Francophonie (OIF).

AES pia imetangaza mpango wa kuunda jeshi la pamoja la wanajeshi 5,000 kupambana na tishio la ugaidi katika eneo hilo. Hatua nyingine ni pamoja na uzinduzi wa pasipoti ya pamoja, na televisheni ya mtandaoni itakayosaidia kupambana na upotoshaji wa habari.