Watu wanaoshukiwa kuwa na silaha wameua watu 52 nchini Nigeria
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i124796-watu_wanaoshukiwa_kuwa_na_silaha_wameua_watu_52_nchini_nigeria
Takriban watu 52 wameuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa baada ya magenge yenye silaha kufanya mashambulizi katikati mwa Nigeria.
(last modified 2025-04-05T10:49:43+00:00 )
Apr 05, 2025 10:49 UTC
  • Watu wanaoshukiwa kuwa na silaha wameua watu 52 nchini Nigeria

Takriban watu 52 wameuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa baada ya magenge yenye silaha kufanya mashambulizi katikati mwa Nigeria.

Farmasum Fuddang, mkuu wa Baraza la Maendeleo ya Utamaduni la Bokkos Vanguard amethibitisha habari hiyo mbele ya waandishi wa habari kwa kusema: "Mashambulizi hayo ya tangu Jumatano usiku yamesababisha hofu katika jamii huko Bokkos katika Jimbo la Plateau. Washambuliaji waliwafyatulia risasi kiholela wakazi wa eneo hilo na kuteketeza kwa moto nyumba zao."

Fuddang anaongoza zoezi la watu kujitolea katika kuingia kwa tabu kwenye vichaka vya maeneo ya karibu kutafuta miili ya watu waliouwa. "Takriban watu 31 walizikwa kwenye kaburi la umati siku ya Alhamisi," amesema.

Fuddang aidha amesema: Siku ya Alkhamisi, miili ya vijana watano ilipatikana katika kijiji cha Hurti, miili mingine 16 ilipatikana wakati wa msako kwenye vijiji kadhaa vya eneo la Bokkos.

Hadi hivi sasa haijajulikana sababu ya umwagaji huo mkubwa wa damu. Bokkos ni moja ya maeneo yanayoshambuliwa mara kwa mara na watu wenye silaha katika Jimbo la Plateau nchini Nigeria.

Katika taarifa yake, serikali ya Jimbo la Plateau ililaani mashambulizi hayo, ikisema vyombo vya usalama tayari vimewakamata baadhi ya washukiwa wanaohhusika na mashambulizi hayo.

Mashambulizi ya kutumia silaha yamekuwa tishio kubwa la usalama katika mikoa ya kaskazini na katikati mwa Nigeria. Vitendo vya mauaji na utekaji nyara vimeongezeka sana katika miezi ya hivi karibuni.