Rais Ruto wa Kenya amsamehe mtu aliyemrushia kiatu Migori
Rais William Ruto amemsamehe mtu aliyemrushia kiatu wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika Kehancha, Kuria Magharibi, Kaunti ya Migori, siku ya Jumapili.
Akizungumza na wanahabari jijini Nairobi, Msemaji wa Serikali Isaac Mwaura amesema kuwa Rais Ruto ameonyesha moyo wa ukarimu kwa kuwasamehe waliohusika.
Mwaura amesema: "Hili halikubaliki kabisa! Ni tabia gani tunawafundisha watoto wetu? Hata hivyo, Rais wetu, akiwa na moyo mkunjufu, amewasamehe waliohusika."
Hata hivyo, hakuthibitisha kama watu waliokuwa kizuizini wameachiliwa kufuatia hatua hiyo ya Rais ya msamaha.
Mwaura pia amewakemea wanaofanya mzaha au kusambaza meme mitandaoni kuhusu tukio hilo, akisema kuwa hatua hizo ni za kisaliti na ukosefu wa heshima kwa uongozi wa taifa.
Ameongeza kuwa: "Taasi ya urais lazima iheshimiwe kwa gharama yoyote. Haijalishi nani aliyeko madarakani kwa sasa. Inasikitisha kuwa kuna watu wanafanya mzaha kuhusu tukio hili."
Hapo awali, familia ya Paul Mutongori, ambaye ni mmoja wa wanaume watatu waliokamatwa kutokana na shambulio hilo la kiatu, iliomba msamaha kutoka kwa Serikali kwa niaba ya mtoto wao, ambaye bado yuko kizuizini.
Mama yake aliongea kwa uchungu akisema alimfundisha nidhamu kubwa mwanaye na kuongeza kuwa, tukio hilo limemfanya ashtuke na kuingiwa na hofu kwa sababu Paul bado yuko chini ya ulinzi wa polisi.
Jumatatu ya jana, polisi katika Kituo cha Polisi cha Kehancha, walithibitisha kuwakamata washukiwa watatu wa kiume wenye umri wa miaka 18, 20 na 22 kuhusiana na tukio hilo lililohusisha kuzomewa Rais William Ruto.