Benki Kuu za EAC zakadiria ukuaji wa uchumi wa asilimia 5.8 mwaka 2025
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i126210-benki_kuu_za_eac_zakadiria_ukuaji_wa_uchumi_wa_asilimia_5.8_mwaka_2025
Benki Kuu za nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) jana Ijumaa zilikadiria kuwa, uchumi wa ukanda huo kwa mwaka huu wa 2025 utakuwa kwa asilimia 5.8.
(last modified 2025-12-29T02:35:25+00:00 )
May 10, 2025 05:41 UTC
  • Benki Kuu za EAC zakadiria ukuaji wa uchumi wa asilimia 5.8 mwaka 2025

Benki Kuu za nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) jana Ijumaa zilikadiria kuwa, uchumi wa ukanda huo kwa mwaka huu wa 2025 utakuwa kwa asilimia 5.8.

Kamau Thugge, gavana wa Benki Kuu ya Kenya ambaye pia ni mwenyekiti wa Kamati ya Masuala ya Fedha ya EAC amesema kuwa, tathmini hiyo itategemea kuendelea ufanisi katika sekta ya kilimo na huduma.

Thugge amesema hayo wakati wa mkutano wa 28 wa kawaida wa Kamati ya Masuala ya Fedha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki uliohudhuriwa na magavana wa benki kuu kutoka Burundi, Kenya, Uganda, Tanzania, Somalia, Rwanda na Sudan Kusini.

Benki Kuu za EAC zimesema kuwa, licha ya kuweko mtazamo chanya wa ukuaji wa uchumi, lakini hatari bado ipo, hasa kutokana na mvutano wa kibiashara wa kimataifa, wasiwasi wa kijiografia na mabadiliko ya hali ya hewa.

Magavana hao wamesema kuwa wastani wa mfumuko wa bei katika ukanda wa Afrika Mashariki ulipungua hadi asilimia 9 mwaka 2024 kutoka asilimia 11.2 mwaka 2023, jambo ambalo linaonyesha athari za sera za fedha, uboreshaji wa upatikanaji wa chakula kutokana na hali nzuri ya hewa na kupungua bei za bidhaa duniani. Mfumuko wa bei unatarajiwa kuendelea kudhibitiwa kwenye nchi nyingi za ukanda huo katika mwaka huu wa 2025.

Vilevile amesema kukwa, sera za kiuchumi katika ukanda ya EAC zimeendelea kuwa thabiti licha ya misukosuko ya kimataifa hasa sekta za kilimo, huduma, madini na mafuta. Mkutano huo umechunguza pia hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa mkakati wa kuwa na Umoja wa Fedha wa Afrika Mashariki ifikapo mwaka 2031.