Madaktari Wasio na Mipaka: Kiasi cha misaada kwa Gaza ni kichekesho
Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka (MSF) limetangaza katika taarifa yake jana (Jumatano) kwamba kiasi cha misaada ambayo utawala wa Israel umeruhusu kuhamishiwa Ukanda wa Gaza ni kichekesho.
Kwa mujibu wa Al-Mayadeen, katika taarifa yake, Madaktari Wasio na Mipaka wameulaani utawala wa Israel kwa kuhamishia kiasi cha kejeli cha misaada ya kibinadamu huko Gaza ili kuepuka kulaaniwa kwa hatua yake ya kuwabakisha na njaa kwa makusudi bwakazi wa Ukanda huo.
Shirika hilo lilisema kuwa hatua ya Israel ya kukubali kupeleka kiasi kidogo na kisichotosha cha misaada huko Gaza inaashiria kuwa inakusudia kujinasua na tuhuma za kuwatesa kwa njaa wakazi wa Gaza.
Madaktari Wasio na Mipaka wamesisitiza kuwa, kiasi cha misaada ambayo Israel imeruhusu kupelekwa Gaza ni kifuniko tu cha kujifanya kuwa mzingiro umekwisha.
Shirika hilo pia limesisitiza kuwa Israel lazima ikomeshe mzingiro wa Gaza na kuacha kuharibu miundombinu yake ya afya kama sehemu ya operesheni yake ya kulisafisha eneo hilo kikaumu.
Wakati huo huo, ripoti mbalimbali za Umoja wa Mataifa zinaonyesha kuwa, uhaba mkubwa wa chakula katika Ukanda wa Gaza umefikia kiwango cha janga la njaa.
Mtandao wa Kimataifa wa Kupambana na Migogoro ya Chakula umetangaza kuwa uhaba mkubwa wa chakula huko Gaza umefikia kiwango kibaya zaidi cha "janga na njaa."
Mtandao huo umesema kuwa, mwaka 2024, watu milioni 295.3 katika nchi 53 kati ya 65 au maeneo yaliyoshughulikiwa na utafiti huo walikabiliwa na viwango vya juu vya uhaba wa chakula. Idadi hii takriban ni watu milioni 13.7 zaidi ikilinganiishwa na mwaka wa kabla yake wa 2023.