Jeshi la Nigeria laokoa watu 76 waliokuwa wametekwa nyara, wamo wanawake na watoto
Maafisa wa serikali ya Nigeria wamesema, jeshi la anga limeokoa watu 76 waliokuwa wametekwa nyara, wakiwemo wanawake na watoto.
Kwa mujibu wa maafisa hao, uokoaji huo unafuatia shambulio la anga lililofanywa dhidi ya ngome ya majambazi katika Bonde la Pauwa kaskazini-magharibi mwa Jimbo la Katsina.
Operesheni hiyo ilikuwa sehemu ya msako wa kiongozi wa genge moja anayejulikana kama Babaro, ambaye amehusishwa na shambulio la wiki iliyopita lililolenga msikiti mmoja wa jimbo hilo.
Imeelezwa kuwa, kwa akali mtoto mmoja alifariki wakati wa operesheni ya uokoaji lakini maafisa hawakusema ikiwa kulikuwa na majeruhi wengine kati ya waliookolewa au wanachama wa genge hilo la majambazi.
Shambulio hilo la anga linaashiria mafanikio katika juhudi za kusambaratisha mitandao ya wahalifu kwenye eneo la kaskazini-magharibi mwa Nigeria ambako magenge yenye silaha yamekuwa yakitesa jamii za vijijini kwa miaka mingi sasa.../