Ripoti: Mashambulizi ya wanamgambo yameshadidi eneo la Sahel Afrika
Mashambulizi ya wanamgambo wenye silaha yanaripotiwa kushadidi katika eneo la Sahel Afrika.
Ripoti zinaonyesha kuwa, wanamgambo katika kanda ya Sahel barani Afrika wamezidisha maradufu mashambulizi yao katika miaka ya hivi karibuni.
Kulingana na uchambuzi wa shirika la habari la AFP na pia data kutoka shirika la ACLED, hali hiyo imesababisha vifo vya watu 77,000.
Mashirika hayo yamebainisha kuwa, makundi yenye mafungamano na mtandao wa kigaidi wa Al-Qaeda yanafanya mashambulizi kote eneo hilo kuanzia Mali, Burkina Faso, Niger, Nigeria hadi mipaka ya Senegal.
Charlie Werb, mchambuzi katika shirika la ACLED ametahadharisha kuwa mzozo wa usalama katika kanda ya Sahel ni tete na hakuna suluhisho la haraka.
Itakumbukwa kuwa, hivi karibuni, Umoja wa Mataifa ulikadiria kwamba, mtandao wa Al-Qaeda pamoja na Kundi la Daesh wana kati ya wanamgambo 7,000 na 9,000 katika kanda hiyo huku kundi jingine kwa jina ISWAP likiwa na kati ya wanamgambo 8,000 hadi 12, 000.
Wakati huo huo, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) limetoa wito wa kutekelezwa juhudi za kimataifa haraka iwezekanavyo ili kukabiliana na mgogoro unaoongezeka wa wakimbizi katika eneo la Sahel barani Afrika, ambapo takriban watu milioni 4 wamelazimika kuhama makazi yao huko Burkina Faso, Mali, Niger na katika nchi nyingine jirani.