BRICS, hatua inayofuata ya Iran kujiunga na jumuiya za kieneo
Mkutano wa marafiki wa Jumuiya ya BRICS ulianza Julai 24 huko Johannesburg, Afrika Kusini, na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ikiwa moja ya nchi zilizoomba uanachama katika jumuiya hiyo, ni mmoja wa wageni muhimu wa mkutano huo.
Ali Akbar Ahmadian, Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran, mbali na kushiriki na kutoa hotuba katika kikao hicho cha marafiki wa BRICS, pia atakutana na kuzungumza na baadhi ya viongozi wenzake kando ya mkutano huo.
Mchakato wa maendeleo ya kiuchumi na kiviwanda ya nchi wanachama wa BRICS unaonyesha kwamba msingi wa harakati na falsafa ya kuundwa kundi hili, kama jumuiya inayoinukia kwa madhumuni ya kuwa na nafasi katika ulimwengu wa baadaye wa kambi kadhaa zenye ushawishi, ni kukabiliana na mfumo unaotawala sasa kimataifa. Kwa sasa nchi 22 zimeomba rasmi uanachama wa BRICS na nyingine 22 zimeonyesha nia ya kujiunga na jumuiya hiyo.
Iran ni miongoni mwa nchi za kwanza kuomba uanachama katika kundi la BRICS, lakini nchi wanachama bado hazijabainisha kikamilifu vigezo vya wanachama wapya kuweza kujiunga na kundi hilo. Mambo kama vile pato kumla la taifa, idadi ya watu, eneo, akiba ya maliasili, nafasi ya kisiasa na kiusalama katika eneo na dunia, na mahusiano na nchi wanachama ni miongoni mwa vigezo vya kukubaliwa wanachama wapya katika BRICS. Kufikia sasa wanachama wote wa BRICS wameunga mkono na kukaribisha uanachama wa Iran katika kundi hilo, na hasa China na Russia zimesisitiza haja ya wanachama wapya kujiunga ambapo zinaichukulia Iran kuwa miongoni mwa nchi zenye uwezo mkubwa wa kujiunga na kundi hilo la kiuchumi.
Kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambayo hivi karibuni imejiunga na Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai, kujiunga na BRICS ni hatua mpya katika kuimarisha uhusiano wa kisiasa na kibiashara na mashirika ya kieneo. Kutokana na kuwa na nusu ya idadi ya watu duniani na kati ya asilimia 25 hadi 28 ya uwezo wa kiuchumi duniani, pamoja na utajiri mkubwa wa rasilimali ya watu na maliasili, kundi la BRICS lina uwezo mkubwa wa kuathiri uchumi wa dunia. Kwa sababu hiyo, kundi la BRICS linaweza kuchukuliwa kuwa fursa nzuri kwa Iran, ambayo iko chini ya vikwazo vya kiuchumi vya upande mmoja vya Marekani.
Wakati huo huo, uanachama wa Iran ambayo ni mmoja wa wazalishaji wakubwa wa nishati ulimwenguni unaweza kuchukuliwa kuwa fursa nzuri na muhimu kwa BRICS. Pia eneo la kipekee la kijiografia la Iran na uwezo wake katika usafirishaji wa bidhaa na biashara ni jambo jingine muhimu ambalo linaivutia sana jumuiya na BRICS kuhusiana na Iran. Faida nyingine muhimu ya kujiunga na BRICS hasa kwa Iran na Russia ambazo zimewekewa vikwazo vya Magharibi ni kujitenga na matumizi ya dola kama sarafu ya kawaida ya biashara kimataifa na kuanzishwa Benki ya BRICS inayoitwa "Benki ya Maendeleo Mapya." Benki hiyo ambayo inatajwa kuwa ya maendeleo ya kimataifa, ina mfumo wa arifa za malipo ambao ni mbadala wa SWIFT ya Marekani.
Kwa ujumla, Iran kujiunga na BRICS inaweza kuwa hatua chanya na madhubuti katika kuimarisha nafasi ya Iran duniani. Kujiunga na BRICS pia kunaweza kusaidia katika kupunguza mivutano ya kieneo na kuongeza nguvu ya kimataifa ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Iran pia inaweza kutumia uwezo na fursa za kundi hili kwa ajili ya kuimaisha maendeleo yake ya kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni.
Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alisema mapema katika mkutano wa video wa viongozi wa nchi za BRICS uliofanyika Juni 2022 kwa uenyeji wa China kwamba: Mienendo inayokinzana kimataifa, misimamo ya upande mmoja, utaifa na changamoto kama vile vikwazo vya kiuchumi zinatoa udharura wa kuundwa na kuimarishwa taasisi mpya pembeni ya Umoja wa Mataifa ili kuheshimiwa tawala na maslahi ya mataifa. Hayo yote ni kwa shabaha ya kufikiwa lengo la kubuniwa "jamii ya wanadamu yenye mustakabali wa pamoja."