Wanafiki wa MKO kufikishwa katika Mahakama ya Jinai ya Tehran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i100546-wanafiki_wa_mko_kufikishwa_katika_mahakama_ya_jinai_ya_tehran
Mahakama Kuu ya Jinai ya Mkoa wa Tehran inatazamiwa kuanza kusikiliza kesi za wanachama watoro zaidi ya 100 wa kundi la kigaidi la Munafikin (MKO) ambalo limefanya mauaji ya makumi ya maelfu ya wananchi wa Jamhuri ya Kiislamu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 01, 2023 01:04 UTC
  • Wanafiki wa MKO kufikishwa katika Mahakama ya Jinai ya Tehran

Mahakama Kuu ya Jinai ya Mkoa wa Tehran inatazamiwa kuanza kusikiliza kesi za wanachama watoro zaidi ya 100 wa kundi la kigaidi la Munafikin (MKO) ambalo limefanya mauaji ya makumi ya maelfu ya wananchi wa Jamhuri ya Kiislamu.

Kwa mujibu wa kesi iliyowasilishwa katika mahakama hii, wanachama 104 wa kundi linalojiita Mojahedin Khalq (MKO) ambalo kimsingi ni kundi la wanafiki na magaidi, watapandishwa kizimbani.

Taarifa ya korti hiyo imesema iwapo mawakili wa magaidi hao hawataarifishwa au kujiarifisha, basi chombo hicho cha sheria kitalazimika kutoa uamuzi unaoendana na sheria, dhidi ya magaidi hao wa kundi la MKO, wenye historia ya kufanya jinai za kutisha na za kinyama.

Katika orodha iliyochapishwa kuna majina ya magaidi kama vile Masoud na Maryam Rajavi na Mehdi Abrishamchi ambao ni vinara  wakuu wa kundi la MKO ambao wamekuwepo tangu siku za mwanzo za uhalifu wa kundi hilo la kigaidi baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu mwaka 1979.

Kundi hilo la wanafiki ambalo hivi sasa linapata hifadhi huko Albania chini ya uungaji mkono wa Marekani, ndilo chimbuko la usaliti na jinai ikiwemo kutangaza vita vya silaha dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kufanya mauaji dhidi ya maafisa wa serikali, kutekeleza milipuko ya mabomu nchini, kuungana na utawala wa Saddam na usaliti mwingine mwingi wa kisiasa na kiujasusi.

Baada ya kushindwa wanafiki hao katika oparesheni za vikosi vya usalama vya Iran katika muongo wa 80 na pia kutokana na ushirikiano mkubwa wa kundi hilo na utawala dhalimu wa Saddam, karibu wanachama wake wote waliondoka Iran na kupewa makazi huko Iraq na baada ya utawala wa Saddam kuangushwa walipata hifadhi katika nchi ndogo ya Albania barani Ulaya. Kwa hivyo, magaidi hao hivi sasa hawana uhusiano rasmi na wa kisheria na Iran  lakini kwa sababu idadi kubwa ya magaidi wa MKO wanaishi Ulaya, inawezekana na ni muhimu kufuatilia jinai za kundi hilo kupitia mahakama za Iran na taasisi za kimataifa.

Marekani ni muungaji mkono mkuu wa magaidi wa MKO

Kwa kuzingatia hilo, kufunguliwa kesi mahakamani dhidi ya kundi hilo na wanachama wake inapaswa kuzingatiwa kuwa ni hatua muhimu, kwani pamoja na kuonesha uzito ambao Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inalipa suala la kukabiliana na magaidi, inaweza kutoa pigo kali kwa kundi hilo sambamba na kuwashinikiza waungaji mkono wake wa kigeni.

Kwa maneno mengine, iwapo hatua za kisheria za kushughulikia jinai za kundi hili zitatekelezwa kwa umakini mkubwa nchini Iran na pia katika majukwaa ya kimataifa na kuambatana na hatua zinazofaa za kidiplomasia, zinaweza kuwa na matokeo madhubuti katika mwelekeo wa kuwadhoofisha na kuwaadhibu magaidi hao.

Mwezi Juni mwaka huu, wakati habari ya  polisi wa Albania kuvamia kambi ya MKO huko Tirana ilipotangazwa, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran aliashiria hatua hii ya serikali ya Albania dhidi ya magaidi hao na kueleza kuridhika kwake huku akibaini kuwa: “Albania imediriki kuwa Iran imekuwa ikisema ukweli.”

Katika sehemu nyingine ya kauli yake, Nasser Kanani aligusia kadhia  ya kurejeshwa wanafiki hao nchini Iran na kusema: “Matarajio ya Iran kutoka kwa nchi zinazowapa hifadhi MKO  ni kwamba wakabidhiwe serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa mujibu wa sheria na kanuni za kimataifa."

Iran pia imetuma maombi kwa nchi kadhaa ikitaka kukamatwa na kurejeshwa Iran kwa idadi kubwa ya magaidi wa MKO kupitia njia zilizopo za mahakama na polisi ya kimataifa. Ni wazi kuwa, katika miezi ya hivi karibuni, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imezidisha hatua zake za kuwarejesha na kuwafungulia mashtaka magaidi hao wa MKO  kwa njia mbalimbali. Iran imeifahamisha serikali ya Albania msimamo wake  na pia imefanya mashauriano na polisi wa kimataifa INTERPOL sambamba na kuandaa nyaraka zinazohusiana na vitendo vya kigaidi vya MKO. Katika muendelezo wa hatua hizo hivi sasa kesi dhidi ya MKO imewasilishwa mahakamani.

Kuwasilishwa kesi hiyo katika mahakama ya jinai mjini Tehran ni moja ya hatua ambazo zimechukuliwa katika mwelekeo huu na inaonyesha namna kadhia ya kuwafungulia mashtaka na kuwaadhibu vikali magaidi wa MKO inavyofuatiliwa kwa umuhimu mkubwa.