Kudumishwa ustawi katika sekta ya ulinzi ya Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i100722-kudumishwa_ustawi_katika_sekta_ya_ulinzi_ya_iran
Mifumo na zana mpya za kistratijia za Jeshi la Wanamaji la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran IRGC katika nyanya za makombora, ndege zisizo na rubani na vita vya kielektroniki zimezinduliwa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 05, 2023 22:57 UTC
  • Kudumishwa ustawi katika sekta ya ulinzi ya Iran

Mifumo na zana mpya za kistratijia za Jeshi la Wanamaji la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran IRGC katika nyanya za makombora, ndege zisizo na rubani na vita vya kielektroniki zimezinduliwa.

Mifumo na zana hizo ni matokeo ya juhudi za wanasayansi na wataalamu wa Shirika la Anga na Anga za Mbali, Shirika la Viwanda vya Baharini, Shirika la Anga na Viwanda vya Kielektroniki la Wizara ya Ulinzi pamoja na mashirika mengine yenye msingi wa maarifa, sekta binafsi na vituo maalumu vya Jeshi la Wanamaji la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu.

Aina mbalimbali za droni za upelelezi, ukusanyaji habari za usalama, hujuma na mashambulizi, aina tofauti za magari ya msaada na deraya, mifumo ya ukusanyaji habari na mashambulizi ya kielektroniki, ni miongoni mwa mifumo na zana mpya zilizozinduliwa.

Malori mbalimbali ya kurusha makombora ya cruise pamoja na mifumo ya rada, mamia ya makombora ya cruise na balestiki yenye umbali wa kilomita 300 hadi 1000 pia ni miongoni mwa mifumo na zana ambazo zimeongezwa kwenye maghala ya silaha ya Jeshi la Wanamaji la IRGC.

Siku ya Jumatano, katika mazoezi ya Jeshi la Wanamaji katika Kisiwa cha Bumusa, kwa mara ya kwanza, mfumo wa makombora wa cruise wa Qadeer na kombora la balestiki la Fat'h 360 lennye uwezo wa akili bandia lilizinduliwa na kupewa jeshi hilo.

Sehemu ya mazoezi ya karibuni ya Jeshi la Wanamaji la IRGC katika Ghuba ya Uajemi

Kuzinduliwa mifumo na zana mpya za kistratijia za Jeshi la Wanamaji la IRGC sio tu kunaonyesha maendeleo na mafanikio mapya katika sekta ya kijeshi ya Iran, bali pia kunaonyesha kwa mara nyingine kwamba vikwazo na mashinikizo ya pande zote ya maadui si kikwazo kwa maendeleo hayo na kuwa kujitosheleza Iran katika sekta ya ulinzi kunatokana na uwezo wa ndani ya nchi.

Mfumo wa ulinzi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran umeegemezwa kwenye uwezo wa ndani, na tangu wakati wa vita vya kujitetea kutakatifu vya miaka minane vilivyoanzishwa na utawala wa Saddam dhidi ya Iran, Jamhuri ya Kiislamu imeweza kudhamini mahitaji yake ya ulinzi kwa kutegemea uwezo wa ndani wa wataalamu wake.

Hii ni pamoja na kwamba Jamhuri ya Kiislamu iliwekewa vikwazo vya silaha tangu miezi ya kwanza ya Mapinduzi ya Kiislamu, vikwazo ambavyo vimeongezwa makali katika miaka ya hivi karibuni. Kwa kadiri kwamba mbali na mashirika ya kutengeneza silaha, watu binafsi na makampuni mengine ambayo yanahusiana moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja na makampuni hayo pia wamewekewa vikwazo.

Licha ya vikwazo hivyo na hata kuuliwa wanasayansi na vilevile kushambuliwa na maadui vituo vyake vya kijeshi, Iran hivi sasa inaongoza katika eneo katika uzalishaji wa zana za kijeshi na ulinzi kutoka makombora na mifumo ya ulinzi wa anga na ndege zisizo na rubani hadi kwenye manowari zilizo na uzito wa tani elfu kadhaa, ndege za kivita na nyambizi.  Uzalishaji na uimarishaji wa droni zinazotengenezwa ndani ya nchi kama vile Qased, Shahid, Simorgh, Mohajer, na makombora ya balestiki na cruise kama vile Qadr, Sijjil, Fateh, Qaim na Fath, utengenezaji na uimarishaji wa ndege za kivita na upelelezi kama vile Kauthar, Azarakhsh, Saeqa na Yasin, uzalishaji na uboreshaji wa nyambizi na manowari kama vile Fateh, Jamaran na Damavand, pamoja na utengenezaji wa silaha zisizoonekana kwenye rada, ni mifano ya maendeleo ya Iran katika uwanja wa teknolojia ya kijeshi katika miaka ya hivi karibuni.

Ni dhahiri kwamba uwezo wa kuzalisha na kutumia silaha na zana za kivita umeiwezesha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa na nguvu kubwa katika kulinda na kuboresha usalama wake na pia katika kufikia kiwango cha juu cha kuzuia hujuma ya maadui.

Mazoezi ya IRGC katika kisiwa cha Bumusa

Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuimarika utayarifu wa jeshi kunawatia kiwewe na kuwaogopesha maadui kiasi cha kuwafanya wasianzishe hujuma dhidi ya nchi na kusisitiza kuwa: Jamhuri ya Kiislamu haina nia ya kuanzisha vita na mtu yeyote, lakini pamoja na hayo inapasa kuongeza uwezo wake ili adui si tu asithubutu kuishambulia Iran, bali pia alazimike kuondoa kivuli cha vitisho dhidi ya taifa la Iran kutokana na mshikamano, uimara na uwepo madhubuti wa vikosi vya jeshi lake katika uwanja huo.