Iran na Muqawama zilivyoshika mpini wa masuala ya eneo la Asia Magharibi
Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) ameashiria uafriti unaofanywa katika kila pembe ya ulimwengu na ubeberu wa dunia ukiongozwa na Marekani na kueleza kwamba, hii leo Marekani inazidi kudidimia na kuyoyoma kuliko ilivyowahi kuwa wakati wowote ule; na leo adui yuko kwenye kilele cha udhaifu.
Meja Jenerali Hossein Salami ambaye alikuwa akihutubia kongamano la 24 la makamanda wa IRGC amesisitiza kuwa, ingawaje diplomasia ni chaguo bora zaidi, lakini diplomasia bila ya kubebwa na nguvu na uwezo haifanyi kazi; na akasema: "leo Mapinduzi ya Kiislamu na mhimili wa Muqawama zina nafasi na sauti ya juu katika kukabiliana na Marekani, Israel ghasibu na washirika wao katika eneo; na mafanikio haya muhimu yamepatikana kwa busara na hekima za Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi na jihadi na istiqama ya Umma wa Kiislamu".
Matamshi hayo ya Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu yanaashiria kwa mara nyingine tena hali halisi ilivyo hivi sasa katika eneo hili ambapo sambamba na kupungua ushawishi wa Marekani kunashuhudiwa kuongezeka kwa nguvu na taathira ya mhimili wa Muqawama na mapambano pamoja na hamu ya nchi za eneo ya kufuata muelekeo wa maelewano na mafahamiano baina yao.
Katika miongo minne iliyopita baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, eneo la Magharibi mwa Asia limeshuhudia zaidi makabiliano ya mikondo na miungano miwili; mmoja wao ni ule unaoongozwa na Marekani na waitifaki wake kama vile utawala wa Kizayuni huku ukiungwa mkono na baadhi ya tawala wafanya mapatano na Israel; mkondo ambao unalenga kulinda maslahi ya Magharibi na kudhoofisha nchi zenye mielekeo huru. Muungano na mkondo wa pili ni wa Muqawama, ambao mhimili wake mkuu ni Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na washirika wake ni pamoja na Syria, Yemen, Iraq, Hizbullah ya Lebanon na makundi kama vile Hamas na Jihadul-Islami; muungano ambao dira yake kuu ni kutetea piganio tukufu la Palestina, kukabiliana na mfumo wa ubeberu na kupinga uwepo wa maajinabi wavamizi na maghasibu katika eneo.
Licha ya hatua za madola mbalimbali ya eneo na ya nje ikiwemo Marekani za kutaka kuzisambaratisha au kuzidhoofisha nchi na makundi yenye misimamo huru yenye mfungamano na mhimili wa Muqawama; nchi hizo na makundi hayo yamezidi kuwa na nguvu kadiri siku zinavyosonga mbele na kuonyesha kuwa na uwezo mkubwa wa kuathiri matukio na mabadiliko yanayojiri katika eneo la Asia Magharibi; kwa kadiri kwamba, mabadiliko yanayojiri hivi sasa katika eneo hili yanafuata mkondo unaokinzana na matakwa ya Marekani na utawala wa Kizayuni.
Wakati huo huo, nguvu na uamrishaji wa kisiasa na kiuchumi wa Magharibi ikiongozwa na Marekani unaendelea kupungua, huku ulimwengu ukielekea kwenye muundo wa kambi kadhaa. Nchi za eneo la Magharibi mwa Asia zinafuata muelekeo wa kushirikiana na kupunguza utegemezi kwa madola ya kigeni. Kurejeshwa uhusiano wa kidiplomasia wa Saudia na Iran, mawasiliano ambayo nchi nyingine za Kiarabu za eneo la Ghuba ya Uajemi zimefanya na Iran ili kumaliza tofauti zao, pamoja na kubadilika misimamo ya nchi za Kiarabu kuhusiana na Syria ni miongoni mwa matukio yanayoonyesha kuwa hata zile nchi ambazo hadi sasa zilikuwa tegemezi kwa Marekani hasa katika masuala ya usalama, hivi sasa zimeonyesha dhamira ya kubadilisha muelekeo huo na kupiga hatua kuelekea kwenye ushirikiano na majirani zao na kutumia mbinu na taratibu za kikanda kwa ajili ya kutatua matatizo yao.
Ni wazi kwamba siasa na sera za nje za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa muongozo wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu zimekuwa na mchango na nafasi muhimu na athirifu katika kuzielekeza nchi za Kiislamu za eneo kwenye mkondo wa maelewano na vilevile katika kuimarisha kambi ya Muqawama. Kwa kustawisha uhusiano wa kisiasa, kiuchumi, kiutamaduni na kiusalama na majirani zake, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeandaa mazingira mwafaka ya kusuluhisha tofauti na vilevile kukabiliana na vitisho vya Marekani na Wazayuni; na matokeo yake, ambayo yanashuhudiwa hivi sasa, ni kushindwa Marekani katika eneo na kuongezeka zaidi ushawishi wa mhimili wa Muqawama katika matukio yanayojiri hivi sasa hasa yale yanayoshuhudiwa katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina.../