Kushindwa vyombo vya habari vya upinzani kuibua machafuko nchini Iran
Katika kipindi kisichopungua mwezi mmoja uliopita vyombo vya habari vya aduii vilipanga na kuratibu njama za kuibua ghasia na machafuko nchini Iran; hata hivyo miji mbalimbali ya Iran katika masiku ya karibuni imeshuhudia hali ya amani na utulivu.
Machafuko ya mwaka mmoja uliopita nchini Iran yalifuatia kifo cha binti kijana wa Kikurdi. Mahsa Amini alitumiwa haraka kama chambo cha kuibua ghasia na fujo kubwa hapa nchini hususan katika maeneo ya mpakani. Ghasia na machafuko hayo yaliendelea kwa zaidi ya siku 100 katika baadhi ya miji ya Iran. Hatimaye mradi huo wa kuibua machafuko nchini Iran uligonga mwamba. Hivi sasa vyombo hivyo vya maadui na mabwana zao vinajaribu kupiga ngoma za kuibua machafuko mengine nchini Iran njama ambazo zimeshindwa na kufeli kwa urahisi ikilinganishwa na mwaka uliopita. Hii ni kwa sababu, mipango yao haijaungwa mkono hata kidogo na wananchi ndani ya Iran.
Hapana shaka kwamba, sababu kuu ya kushindwa maadui wa Jamhuri ya Kiislamu ni kutowafahamu vyema wananchi na mfumo wa Kiislamu. Mfumo wa Kiislamu uliasisiwa kwa mujibu wa matakwa ya wananchi wa Iran; na ni jambo la kawaida kwamba licha ya kuwepo malalamiko hasa katika sekta ya uchumi, wananchi hawatakengeuka na kwenda kinyume na malengo ya Mapinduzi ya Kiislamu. Ni wazi kuwa, maadui wa Iran hawana uwezo wa kuelewa umoja na mafungamano uliopo kati ya wananchi na mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu, na wanakariri tu baadhi ya vijidosari na mapungufu.
Sababu nyingine kubwa iliyopelekea kushindwa njama za kuibua machafuko nchini Iran ni kufichuliwa sura halisi ya maadui na tofauti kubwa zinazojiri baina yao. Wananchi katika muda wa miezi 9 iliyopita wametambua kuwa lengo kuu la maadui hao si kuwatetea wananchi, bali ni kutaka kuingia madarakani kwa gharama yoyote hata kwa kuigawa ardhi ya Iran; suala ambalo ni mstari mwekundu kwa wananchi wa Iran. Mbali na hilo, imebainika wazi kwamba, maadui hao wanaaotaka kushikama madaraka ya nchi, hawana ushawishi wowote katika uga wa kisiasa, hawana ufahamu wa mitazamo na fikra za kidini na kisiasa za wananchi wa Iran na wanatawliwa na hitilafu kubwa baina yao.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi mwaka mmoja uliopita alisisitiza mara kadhaa ulazima wa kufuatilia na kuwadhaminia wananchi mahitaji yao na kubainisha malengo ya adui ya kutaka kuibua ghasia na fujo hapa nchini. Sisitizo la Kiongozi Muadhamu la kuwepo umoja na kudhaminiwa usalama wa taifa katika ziara yake ya karibuni huko Sistan Baluchistan na Khorasan Kusini linaweza kutathminiwa katika uwanja huo.
Nukta ya mwisho ni kuwa, adui katika ghasia na fujo za mwaka jana alitaka kuwahadaa wananchi; hata hivyo, kama kawaida wananchi wenye busara wa Iran walitambua vyema njama hizo na uhakika kwamba wanapaswa kuwa wazalendo na kufanya kazi kwa bidii kwa ajili ya kuijenga nchi yao wao wenyewe na si kuwaamini vibaraka wa nchi za kigeni.