Mitazamo wa Kiongozi Muadhamu; kujihami kutakatifu kumetanua mipaka ya muqawama
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameonana na kuhutubia mjumuiko wa vinara, familia za mashahidi, wasanii, waandishi, wasaidizi, maveterani na wanaharakati wa masuala ya vita vya kujihami kutakatifu (vya baina ya Iran na utawala wa zamani wa Iraq) na kutilia mkazo udharura wa kuendelezwa njia ya muqawama.
Katika hotuba yake kwenye mjumuiko huo jana Jumatano tarehe 20 Septemba, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amesisitiza kuwa, kuweza taifa la Iran kulinda ardhi yote ya nchi, kubainisha uwezo na nafasi kubwa ya taifa la Iran, kutanuliwa mipaka isiyo ya kijiografia ya Jamhuri ya Kiislamu na kutia nguvu maana ya utamaduni wa muqawama ndani ya Iran na duniani kiujumla, ni matunda ya kujihami kwa pamoja wananchi wote wa Iran mbele ya kambi ya kibeberu ulimwenguni na Saddam khabithi.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa hotuba hiyo wakati huu wa kukaribia maadhimisho ya Wiki ya Kujihami Kutakatifu nchini Iran na kusema kuwa, kujaribu kuyasambaratisha Mapinduzi ya Kiislamu na Jamhuri ya Kiislamu na kuteka baadhi ya maeneo ya Iran ndiyo yaliyokuwa malengo makuu ya maadui katika vita ilivyolazimishwa Iran kupigana na utawala wa zamani wa Iraq.
Amesisitiza kuwa, ushindi wa Mapinduzi matukufu ya Kiislamu nchini Iran kilikuwa ni kitu kipya cha kipekee kwani wakati huo hakukuwa na mapinduzi yoyote yaliyokuwa yametokea duniani kwa msukumo wa kidini na kwa nguvu za wananchi na ndio maana mabeberu wa dunia walifanya na wanaendelea kufanya njama zao zote kujaribu kuzima harakati hiyo mpya yaani Jamhuri ya Kiislamu na demokrasia ya kidini.
Kama alivyoashiria Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran na kufanikiwa Mapinduzi hayo kusambaratisha mlingano wa kiistikbari dunani, taifa hili la Kiislamu muda wote limekuwa chini ya mawimbi ya chuki na hamaki za maadui na vibaraka wao. Maadui hao ikiwemo Marekani wanatumia nguvu zao zote kujaribu kuyavunja nguvu Mapinduzi ya Kiislamu; kama walivyofanya kulibebesha taifa la Iran vita vya miaka minane vilivyoanzishwa na utawala wa Saddam. Maadui hao waliusheheneza silaha utawala vamizi wa Saddam, waliliwekea taifa la Iran vikwazo vikali na vikubwa na kufanya mpaka mauaji ya kigaidi dhidi ya makamanda wa muqawama ili kujaribu kuonesha kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetengwa na haina lolote la maana inaloweza kufanya, lakini wameshindwa kufikia lengo lao hata moja.
Moja ya matunda muhimu ya miaka ya kujihami kutakatifu, ni taathira za moja kwa moja za vita hivyo katika kuiletea Iran ya Kiislamu usalama imara mbele ya vitisho vya kila namna vya kijeshi, kiusalama na hata vya kisiasa na kiuchumi; vya maadui, ambavyo katika miaka yote hii ya baada ya vita vya kujihami kutakatifu na licha ya kuweko mashinikizo, uadui wa wazi vikwazo na vitisho vya kila upande, taifa la Iran limeendelea kuwa imara na lina nguvu kubwa za kijeshi kiasi kwamba maadui pamoja na majigambo yao, lakini wanaogopa kuanzisha vita vya kijeshi na taifa hili.
Ukweli wa mambo ni kuwa, Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yana sifa nyingi za kipekee ambazo ni pamoja na kushikamana na dini na masuala ya kimaanawi katika siasa zake, katika kukabiliana na madola ya kibeberu na watawala vibaraka, kufufua utamaduni wa muqawama na moyo wa kuwa tayari kufa shahidi, kupigania uadilifu, kutilia mkazo mshikamano wa mataifa ya dunia, kuwa na nafasi wanayotakiwa kuwa nayo wananchi kwenye maamuzi ya nchi, kuimarisha Uislamu wa kisiasa pamoja na kuwa na ushawishi katika eneo hili na duniani kwa ujumla. Kwa kweli Mapinduzi haya matukufu yameziathiri nchi na mataifa mengi duniani. Taathira hizo zimeyafanya Mapinduzi ya Kiislamu ya nchini Iran kuwa kigezo kwa mataifa mengine hasa ya wanyonge na yanayopigania kujikomboa kutoka kwenye makucha ya madhalimu na madola ya kibeberu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amesema pia kuwa, suala la kutanuliwa mipaka isiyo ya kijiografia ya Iran ikiwemo mipaka ya kifikra na maarifa, ni miongoni mwa matunda mazuri ya kipindi cha vita vya kujihami kutakatifu. Athari zake kubwa zinaonekana katika harakati ya kimataifa ya muqawama huko Palestina, Syria, Iraq na maeneo mengine duniani. Mafanikio ya taifa la Iran yana washitiri wengi pia katika maeneo mbalimbali ya Asia, Afrika, Amerika ya Latini na mataifa mbalimbali ulimwenguni.