Umoja wa Kiislamu maandalizi ya kuhuisha adhama ya ustaarabu wa Kiislamu
Mkutano wa 37 wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu umefanyika hapa mjini Tehran. Kama ilivyo ada, mkutano wa kila mwaka wa kimataifa wa Umoja wa Kiislamu umefanyika hapa Tehran kwa mnasaba wa Wiki ya Umoja sambamba na Maulidi ya Mtume (saww).
Mkutano wa mara hii ambao ulifunguliwa na Rais wa Iran, Sayyid Ebrahim Raisi umeehudhuriwa na shakhsia, wanafikkra, wanazuoni, wasomi na wahadhiri wa vyuo vikuu kutoka katika mataifa mbalimbali ya Kiislamu.
Mkutano wa 37 wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu ambao umefanyika chini ya kaulimbiu ya "Ushirikiano wa Kiislamu kwa ajili ya Kufikia Matukufu Pamoja" umehudhuriwa na zaidi ya shakhsia na Maualmaa 3,000 kutoka zaidi ya nchi 41 duniani.
Katika mkutano huu, mada na masuala mbalimbali muhimu yanayohusiana na ulimwengu wa Kiislamu yalijadiliwa. Katika mkutano huu, kamati maalumu zimeundwa kutekeleza malengo hayo na kuondoa vizingiti vya umoja na maendeleo.
Kufikia thamani za pamoja na kuzitambulisha kwa Waislamu na kuwataka kuyazingatia hayo, ndiyo njia muhimu zaidi ya kuendeleza mshikamano na ukuruba baina ya Waislamu.
Kwa kuwa filihali, kaulimbiu kuu ya mkutano huu ni "Ushirikiano wa Kiislamu kwa ajili ya Kufikia Matukufu Pamoja" imepatikana fursa adhimu ambapo kwa maafikiano ya wanafikra na wanazuoni wa Ulimwengu wa Kiislamu, kuyatoa mambo haya ya pamoja ndani ya vyanzo vya Kiislamu na kuyatambulisha kwa Waislamu ili kupitia kwayo jamii ya Kiislamu iweze kupitia hatua kuelekea upande wa mshikamano na katika kalima moja ya "Umma Mmoja" ni mambo ambayo yanaweza kufikiwa tu kupitia kwa wanafikra wa Kiislamu wenye umoja na mshikamano baina yao.
Suala la kukurubisha baina ya madhehhebu za Kiislamu, kukurubisha jamii ya Tawhidi na kukurubisha baina ya fikra za pamoja za wanadamu wote ni moja ya kazi muhimu ambayo inasisitizwa na wanaoitakia kheri jamii inayoshikamana na dini na jamii ya mwanadamu na ni moja ya matumaini na ndoto za wasomi wengi.
Kwa muda wa miaka 37 sasa, mkutano wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu umekuwa ukifanyika mjini Tehran kwa ajili ya kuimarisha umoja na kutatua migogoro na matatizo ya ulimwengu wa Kiislamu, na kuimarisha uwezo sambamba kuongeza nguvu za Waislamu katika nyuga mbalimbali.
Kufuatia tangazo la Wiki ya Umoja lililotolewa na muasisi wa Jamhhuri ya Kiislamu ya Iran, Imam Khomeini, na kwa kuzingatia stratijia ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ya kuimarisha umoja wa Kiislamu baina ya Waislamu, kulichukuliwa uamuzi na maafisa husika wa kufanyika kila mwaka mkutano wa Kimataifa la Umoja wa Kiislamu .
Kipindi hiki cha baina ya tarehe 12 na 17 Mfunguo Sita Rabiul-Awwal kilitangazwa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa ni Wiki ya Umoja na Mshikamano Baina ya Waislamu wote duniani, lengo likiwa ni kuwakusanya pamoja Waislamu wote wa madhehebu na mitazamo tofauti katika Tauhidi na umoja wa Kiislamu.

Kutangazwa tarehe 12 hadi 17 Mfunguo Sita Rabiu al-Awwal kwa jina la Wiki ya Umoja hakujakaribishwa na kupokewa kwa mikono miwili tu katika Iran ya Kiislamu, bali pia katika ulimwengu wa Kiislamu, na kila mwaka katika wiki hii hufanyika hafla mbalimbali za kitamaduni kwa kuhudhuriwa na wanazuoni wa Shia na Sunni kuonyesha umoja na mfungamano wa nyoyo unaotawala baina yao.
Lengo kuu la kufanya hafla maalumu za Wiki ya Umoja ni kuimarisha umoja na mafungamano ya Umma wa Kiislamu katika kivuli cha kuzingatia maneno ya Mwenyezi Mungu kwa ajili ya kuendeleza izza, heshima na utukufu wa Waislamu duniani.
Nbi jambo lisilo na shaka kwamba, siku hizi ni fursa nzuri zaidi ya kuandaa ratiba za kuleta umoja, kubainisha na kufahamisha baraka na udharura wa umoja kwa vijana na watu wote kwa jumla yaani Mashia na Masuni.
Mpango wa Umoja wa Kiislamu kabla ya kuwa ni mpango wa kisiasa, kimsingi ni mradi na mpango muhimu wa kistaarabu. Kuchomoza na kujitokeza ustaarabu wa Kiislamu kunawezekana tu kwa kuweko umoja wa Mashia na Masunni, na ili kufikia hilo ni lazima ulimwengu wote wa Kiislamu uungane na kuwa kitu kimoja.
Nguvu, maendeleo ya kielimu na ustaarabu wa Kiislamu hutegemea kupatikana kwa umoja katika jamii za Kiislamu, na hapana shaka kuwa, kuhuisha ustaarabu wa Kiislamu ni jambo ambalo linawezekana kwa kupitia njia ya kuweko umoja na mshikamano baina ya Waislamu.