Uhusiano wa Iran na China katika serikali mpya ya awamu ya 14
(last modified Wed, 17 Jul 2024 08:37:50 GMT )
Jul 17, 2024 08:37 UTC
  • Uhusiano wa Iran na China katika serikali mpya ya awamu ya 14

Kufuatia kuchaguliwa Masoud Pezeshkian kuwa rais mpya wa Iran, swali linajotokeza hapa kuwa je, uhusiano wa baadaye kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na China utakuwa vipi katika serikali ya awamu ya 14 ya Tehran.

Uhusiano na Ushirikiano wa Iran na China ni miongoni mwa mahusiano ambayo ni muhimu kwa nchi hizi mbili na kwa mataifa yenye nguvu kieneo na kimataifa.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni mojawapo ya mataifa yenye nguvu katika eneo la Asia Magharibi na mojawapo ya wazalishaji na wauzaji wakubwa wa mafuta duniani.

China: Tuko tayari kushirikiana na serikali mpya ya Iran

China pia ni miongoni mwa mataifa yenye nguvu kubwa duniani na mwanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ambayo ina haki ya kura ya turufu katika baraza hilo, na wakati huo huo ni miongoni mwa nchi zinazoagiza mafuta kwa wingi duniani. Licha ya kuwa uhusiano wa nchi hizi unadhamini maslahi yao katika nyanja mbalimbali, lakini pia unatazamwa kwa jicho la wasiwasi na washindani wao wa kikanda na kimataifa.

Marekani ni miongoni mwa mataifa yenye nguvu duniani ambayo yanapinga kustawishwa uhusiano wa Iran na China, kwa sababu kwa upande mmoja inaamini kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inajaribu kukwepa vikwazo kwa kuendeleza uhusiano na China, na kwa upande mwingine, China nayo inajaribu kudhamini maslahi yake ya kiuchumi kwa kuendeleza uhusiano na nchi za Asia Magharibi, ikiwa ni pamoja na Iran, na hivyo kuongeza ushawishi na nafasi yake kieneo na kimataifa.

Licha ya upinzani wote huo na vizuizi vya kila upande vya Marekani, lakini uhusiano wa Iran na China uliendelea kuimarika katika serikali ya hayati Shahid Ebrahim Raisi, ambapo nchi mbili zilitia saini makubaliano na ushirikiano wa kimkakati wa miaka 25.

Kwa kuingia madarakani Masoud Pezeshkian, Rais mteule wa Iran, sasa macho yote duniani yameelekezwa kwenye sera za kigeni za Iran, hasa kuhusu uhusiano wake na nchi kama China.

Katika makala aliyoandika karibuni kuhusu sera za nje iliyochapishwa katika gazeti la Tehran Times, Pezeshkian alisema kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inathamini sana urafiki mkongwe na wa muda mrefu uliopo kati yake na China, na kuwa ina hamu ya kushirikiana zaidi na China katika juhudi za kufikia mfumo mpya wa utawala duniani.

Mtazamo huo wa wazi wa Dakta Pezeshkian unaonyesha wazi kwamba kustawisha uhusiano na kupanua wigo wa ushirikiano na China ni stratijia ya kudumu katika sera za kigeni za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kuwa haibadiliki pakubwa kwa kubadilika serikali mjini Tehran.

Jibu la China kuhusiana na matamshi hayo ya Pezeshkian pia linaashiria hamu kubwa ya Beijing ya kuendeleza hali ya hivi sasa ya uhusiano wake na Iran katika serikali ya awamu ya 14, katika nyanja tofauti.

Kuhusiana na hilo, Lin Jian, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China amesema;

China Lin Jian, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje akielezea nia ya China ya kuimarisha ushirikiano na serikali mpya ya Iran

"China inashukuru ujumbe wa Masoud Pezeshkian, Rais Mteule wa Iran kuhusu uhusiano kati ya Iran na China. Mahusiano ya kirafiki kati ya nchi zetu mbili yanarudi nyuma karne nyingi zilizopita. Katika kipindi cha miaka 50 iliyopita, hasa tangu nchi hizi mbili zianzishe uhusiano wa kidiplomasia, uhusiano baina ya nchi hizi umekuwa ukiimarika kwenye mkondo mzuri na thabiti." Amesema: "Zinapokabiliwa na changamoto tata za kikanda na kimataifa, China na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran zimekuwa zikisaidiana na kusimama pamoja, kuimarisha uaminifu wa kimkakati, kukakuza uhusiano na ushirikiano katika nyanja mbalimbali na kudumisha mawasiliano na uratibu mzuri katika masuala ya kikanda na kimataifa kwa manufaa ya mataifa mawili na pia kuchangia amani na utulivu wa kikanda na wa ulimwengu mzima kwa ujumla.