Kinu cha nyuklia cha Iran chavunja rekodi ya kuzalisha umeme
Kinu cha nyuklia cha Bushehr cha kusini mwa Iran kimevunja rekodi ya kuzalisha umeme kati ya vinu vyote vya nishati hiyo humu nchini ambapo katika kipindi cha siku 60 zilizopita kimeweza kuzalisha megawati 1,395,290 umeme ambao unatosheleza matumizi ya familia milioni 203.
Shirika la habari la FARS limenukuu ripoti ya karibuni kabisa iliyotolewa na uongozi wa sekta ya uzalishaji umeme ya kinu cha nyuklia cha Bushehr cha kusini mwa Iran na kusema kuwa, kuzalisha umeme kwa wingi wa megawati milioni moja na laki tatu na 95,290 katika kipindi cha miezi miwili tu ni rekodi mpya. Umeme huo umeweza kudhamini mahitaji ya wananchi wa mikoa yote ya fukwe za kusini mwa Iran kuanzia mkoa wa Sistan na Baluchistan hadi mkoa wa Khuzestan.
Kinu hicho kilikamilisha mchakato wa kuingizwa fueli nyuklia tarehe 18 Juni mwaka huu na kimeingia kikamilifu katika kazi ya kuzalisha umeme.
Kwa mujibu wa ripoti ya Wizara ya Nishati ya Iran, kiwango hicho cha uzalishaji umeme kimepiku vinu vyote vya nyuklia vya Iran bali kimefunja rekodi ya uzalishaji umeme wa maeneo mengi tu.
Wataalamu mbalimbali wa masuala ya nishati wanasema kuwa, vikwazo ilivyowekewa Iran katika mradi wake wa matumizi ya amani ya nishati ya nyuklia vimewafanya vijana wa taifa hili wajipinde na kufanikiwa kumiliki nishati hiyo kwa asilimia 100 kutokea humuhumu ndani ya Iran. Si hayo tu, hata njama za maadui za kuwaua kigaidi wataalamu wa nyuklia wa Iran hazijalizuia taifa hili la Kiislamu kupiga hatua kubwa katika maendeleo ya nyuklia na mengineyo.