Iran, Malaysia zalaani msaada wa kijeshi wa madola ya Magharibi kwa Israel
Iran na Malaysia zinakubaliana kwamba msaada wa silaha unaotolewa na Marekani na nchi nyingine za Magharibi kwa utawala wa Kizayuni Israel unakinzana na madai yao kuhusu haki za binadamu na pia msaada huo unadhoofisha juhudi za usitishaji vita huko Gaza.
Katika mazungumzo ya simu siku ya Jumatatu, Rais Masoud Pezeshkian wa Iran na Waziri Mkuu Anwar Ibrahim wa Malaysia walijadili matukio ya hivi punde katika eneo la Asia Magharibi, hasa mazungumzo yanayoendelea ya kusitisha mapigano Gaza.
Pande hizo mbili zimesisitiza umuhimu wa kustawisha umoja na mshikamano kati ya mataifa ya Kiislamu ili kupambana na jinai za Israel na kukomesha mauaji ya halaiki katika Ukanda wa Gaza uliozingirwa.
Wamesema kufanyika kwa mkutano wa kilele wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) kutakuwa njia muafaka ya kujadili kadhia ya Palestina.
Israel ilianzisha kampeni yake ya kikatili ya mauaji ya kimbari huko Gaza mnamo Oktoba 7, 2023, baada ya makundi ya wapigania ukombozi wa Palestina kufanya operesheni ya aina yake ya Kimbunga cha Al-Aqsa ya kuwaangamiza Wazayuni ili kulipiza kisasi jinai za miongo kadhaa za utawala wa Israel dhidi ya Wapalestina.
Katika kujibu operesheni hiyo, Israel imewaua zaidi ya Wapalestina 40,000 huko Gaza, wengi wao wakiwa wanawake, watoto na vijana.