SEPAH: Operesheni za Muqawama dhidi ya Israel zitaendelea
Kaimu wa Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH amesema kuwa, maadamu hujuma na jinai za Israel zinaendelea, operesheni za harakati za Muqawama nazo kamwe hazitosimama. Ameongeza kuwa, baada ya Operesheni ya Kimbunga cha al-Aqsa, majigambo ya utawala wa Kizayuni yalisambaratika kikamilifu.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Tasnim, Brigedia Jenerali Mohammad Hossein Falahzadeh amesema hayo katika sherehe za Siku ya Msikiti Duniani mjini Shiraz Iran, wakati alipokuwa anawasilisha ripoti kuhusu hali ya hivi sasa katika eneo la Asia Magharibi, hasa hali ya Palestina na hususan Ghaza. Amesema: Baada ya Operesheni ya Kimbunga cha al Aqsa, majigambo ya utawala wa Kizayuni yalisambaratika kabisa ndio maana Marekani imeamua kutumia nguvu zake zote kujaribu kufufua itibari ya dola hilo pandikizi.
Amesema, kwa msaada kamili wa Marekani, utawala wa Kizayuni ulianza kufanya jinai za kutisha tangu tarehe 7 Oktoba 2023 hadi hivi sasa dhidi ya wananchi wa kawaida huko Ghaza lakini kambi ya Muqawama nayo haikufunga mikono na kuangalia kwa macho tu jinai hizo za Wazayuni , bali harakati za Muqawama za nchi mbalimbali za eneo hili zimeingia vitani kuwasaidia ndugu zao Wapalestina kupitia kushambulia maeneo na maslahi ya utawala wa Kizayuni katika eneo hili.
Amesisitiza kwa mara nyingine kwamba, majibu ya harakati za Muqawama kwa jinai za utawala wa Kizayuni hazitosimama maadamu utawala huo dhalimu unaendelea kufanya jinai dhidi ya Wapalestina hasa wa Ghaza kwa msaada kamili wa madola ya kibeberu yakiongozwa na Marekani.
Naibu huyo wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameeleza kuwa, Muqawama wa Iraq umewaweka Wamarekani vamizi katika kipindi kigumu, wamefanya oparesheni 100 za ndege zisizo na rubani dhidi yao huku Hizbullah ya Lebanon ikiyakwamisha kwenye kinamasi majeshi matatu 3 ya Israel na sasa yamechanganyikiwa kabisa katika hali ambayo Muqawama wa Yemen umeufungia kikamilifu utawala wa Kizayuni Bahari Nyekundu na unaendelea kuusababishia hasara kubwa.