Eslami: Sekta ya nyuklia ya Iran iko katika kiwango cha kimataifa
Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran amesema: Sekta ya nyuklia ya Jamhuri ya Kiislamu ni moja ya fakhari za taifa hili. Shughuli za nyuklia za Iran ni za kiwango cha kimataifa na wale waliokuwa wakibeza na kufifiliza mafanikio hayo, hivi sasa wamelazimika kubadilisha misimmamo yao na kukiri nguvu za Iran katika sekta hiyo muhimu.
Shirika la habari la Tasnim limemnukuu Mohammad Eslami akisema hayo jana jioni mbele ya waandishi wa habari huko Arak (katikati mwa Iran) kusema kuwa, hatua nzuri zimechukuliwa katika kuimarisha sekta ya nyuklia ya Iran.
Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran ameeleza kuwa, kuna fursa zisizohesabika mbele ya mradi huo wa nyuklia na kuongeza kuwa, wafanyakazi wa sekta ya nyukia, wasomi na wahusika wote wana wajibu wa kufanya kazi kijihadi na kwa ari na nguvu kubwa zaidi, ili kustafidi vizuri na fursa hizo.
Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran amesisitizia pia wajibu wa kutumika teknolojia mpya katika uzalishaji na kusema kuwa hivi sasa dunia inaelekea kwenye maendeleo endelevu na suala muhimu zaidi ni kuwa na ufanisi wa hali ya juu na kwenda sambamba na maendeleo ya ulimwengu.
Madola ya kibeberu yamekuwa yakifanya njama za kila namna kujaribu kulizuia taifa la Kiislamu la Iran lisimiliki wala na kunufaika na teknolojia za kisasa zikiwemo za matumizi ya amani na ya kiraia ya nishati ya nyuklia kuanzia kuliwekea vikwazo vya kila namna taifa hili mpaka kuua kigaidi wataalamu na wanasayansi wake, lakini maadui wameshindwa, na hivi sasa teknolojia ya nyuklia ya Iran ni ya kiwango cha kimataifa.