Kiwewe cha Wazayuni katika kusubiri jibu la kushtukiza la Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i115550-kiwewe_cha_wazayuni_katika_kusubiri_jibu_la_kushtukiza_la_iran
Kadiri jibu la Iran kwa kitendo cha kigaidi cha utawala wa Kizayuni wa Israel linavyozidi kuchukua muda mrefu, ndivyo taathira za kimaada, kiroho na kisaikolojia zinavyozidi kuongezeka na kuwaumiza Wazayuni.
(last modified 2024-08-23T06:49:34+00:00 )
Aug 23, 2024 06:49 UTC
  • Kiwewe cha Wazayuni katika kusubiri jibu la kushtukiza la Iran

Kadiri jibu la Iran kwa kitendo cha kigaidi cha utawala wa Kizayuni wa Israel linavyozidi kuchukua muda mrefu, ndivyo taathira za kimaada, kiroho na kisaikolojia zinavyozidi kuongezeka na kuwaumiza Wazayuni.

Kuhusu wakati wa jibu la Tehran kwa utawala wa Israel baada ya kuuawa shahidi Ismail Haniyeh, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Hamas, mwakilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa ametangaza kwamba: Jibu la Iran pengine litakuwa katika wakati, mazingira na kwa namna isiyotarajiwa na utawala huu.

Wasiwasi na mkanganyiko wa kinafsi wa Wazayuni unazidi kuongezeka siku baada ya siku kutokana na jibu la uhakika la Iran kwa mauaji ya hivi karibuni ya Shahidi Ismail Haniyeh akiwa mgeni mjini Tehran, na pia majibu ya harakati ya Muqawama kwa mauaji ya Shahidi Fuad Shukr, aliyekuwa mmoja wa makamanda wa harakati Hizbullah ya Lebanon.

Baada ya mauaji ya kigaidi ya Ismail Haniyeh na Fuad Shukr, maafisa wakuu wa mhimili wa mapambano walitangaza kwamba watalipiza kisasi cha damu za mashahidi hao kutoka kwa utawala wa Kizayuni wa Israel.

Redio ya utawala wa Kizayuni wa Israel imekiri kuwa baada ya kuuawa shahidi Haniyeh, Wazayuni wanasubiri majibu ya operesheni hiyo ya mauaji kwa wasiwasi mkubwa. Ikiashiria barabarani zisizo na watu na wasiwasi unaotawala nyuso za Wazayuni, redio hiyo imefananisha hali hiyo na ile ya kipindi cha mambukizi ya Corona.

Hali ya sasa ya Israel inashabihiana na ya kipindi cha corona kwa woga wa kisasi cha Iran

Vyombo vya habari vya Kizayuni pia vinazungumzia kuvurugika shughuli za vivuko na viwanja vya ndege, kusitishwa safari nyingi za ndege na mkanganyiko wa abiria huko Israel. Idara za ujasusi za utawala huo pia zinajaribu kupata habari za aina, shabaha na wakati wa shambulio la kulipiza kisasi la Iran na kambi ya Muqawama kwa msaada wa washirika wake.

Udhaifu wa kiuchumi, kijeshi, kiusalama, mitandao na wa kijasusi wa utawala wa Kizayuni katika kivuli cha jibu la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Hizbullah na Mhimili wa Muqawama unazidisha wahka na wasiwasi wa Wazayuni. Mbali na changamoto za kijeshi, kiusalama, kiintelijensia na kadhalika, utawala wa Kizayuni wa Israel unakabiliwa na matatizo ya kiuchumi kutokana na vita, hasa oparesheni za jeshi la Yemen katika Bahari Nyekundu, Bahari ya Hindi na Bahari ya Arabia. Uchumi uliokumbwa na mgogoro wa Israel umeingia katika kipindi kipya cha shaghalabaghala na mchafukoge kutokana na vita vya Gaza.

Leo hii, kwa kutilia maanani vita vya Gaza na mlingano mpya wa baharini uliowekwa na Yemen dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel, hakuna meli yoyote inayoruhusiwa kuingia na kutoka kwenye maeneo ya utawala huo kupitia njia ya Bab al-Mandab, hadi mzingiro wa Gaza utakapoondolewa, na chakula, dawa na mahitaji mengine ya kimsingi yakaruhusiwa kuingia eneo hilo.

Awali, baadhi ya vyombo vya habari vilieneza dhana kwamba iwapo mazungumzo ya Doha juu ya kusitisha vita na kubadilishana mateka yatafanikiwa, huenda yakaathiri jibu la Iran kwa ugaidi wa Israel. Hata hivyo ushahidi unaonyesha kuwa, Netanyahu bado anajaribu kukwamisha mazungumzo hayo kwa maslahi yake binafsi, na juhudi za Waziri wa Mambo ya Nje wa utawala wa Biden, hazijazaa matunda.

Upinzani wa Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, dhidi ya usitishaji vita katika Ukanda wa Gaza umeondoa uwezekano wa kufikiwa makubaliano ya kuachiliwa huru mateka wa Kizayuni kwa ajili ya kuachiliwa huru wafungwa wa Kipalestina kutoka katika jela za Israel, na idadi kubwa ya mateka wa Kizayuni wameuawa kutokana na mashambulizi ya kikatili ya utawala huo katika maeneo tofauti ya Ukanda wa Gaza.

Kanali ya 12 ya televisheni ya Israel, ikinukuu chanzo cha kuaminika katika mazungumzo hayo, imesema kwamba: Netanyahu anatoa kipaumbele kwa suala la kuendeleza vita badala ya kurejesha (mateka wa Kizayuni kutoka Ukanda wa Gaza).

Benjamin Netanyahu

Jeshi la Kizayuni, ambalo lilishambulia Ukanda wa Gaza kwa kisingizio cha kukomboa mateka wake, halijaweza kukomboa mateka hao wakiwa hai licha ya kupita zaidi ya miezi kumi ya vita. Si hayo tu, bali jeshi la Israel pia limeua mateka wake waliokuwa wakishikiliwa na harakati za mapambano ya ukombozi huko Gaza, suala ambalo limeibua wimbi kubwa la hasira na maandamano dhidi ya serikali ya Netanyahu.