Iran inaunda makumi ya satelaiti kwa malengo mbali mbali
Mkuu wa Shirika la Anga za Juu la Iran (ISA) Hossein Salariyeh anasema nchi Iran imepata maendeleo ya ajabu katika sekta ya anga katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita na hivi sasa makumi ya satelaiti zinaendelea kuundwa nchini kwa malengo mbalimbali.
Salariyeh alisema siku ya Alhamisi kwamba hivi sasa satelaiti 30 za kiasili zinaendelea kuundwa nchini Iran, ambapo 20 kati ya hizo zinaundwa na sekta ya kibinafsi.
Aidha amebainisha kuwa satelaiti 12 za Iran zimerushwa katika obiti ya sayari ya dunia kwa mafanikio tangu Agosti 2021. Amesema Shirika la Anga za Juu la Iran lina satelaiti 14 zilizopangwa kurushwa.
Salariyeh pia amesema kasi ya kubuni na kutengeneza satelaiti ndani ya nchi imeongezeka kwani Shirika la Anga za Juu la Iran limeanzisha miradi ya pamoja na sekta ya kibinafsi,
Sekta ya anga za juu inazingatiwa kuwa kati ya tasnia yenye teknolojia ya hali ya juu. Licha ya mapungufu yote yanayotokana na vikwazo vya madola hasimu ya Magharibi hasa Marekani, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeweza kumiliki mzunguko kamili wa teknolojia ya anga ya juu. Hii ina maana kuwa, mbali na kuwa na uwezo na kuunda na kurusha satalaiti angani, Iran pia ina kituo cha ardhini cha kupokea data zinazotumwa na satalaiti.
Hivi sasa Iran ni miongoni mwa nchi 10 zinazoongoza duniani katika sekta ya anga za juu duniani na mafanikio hayo ni matokeo ya zaidi ya miongo minne ya jitihada za wataalamu wa nchi hii ya Kiislamu.