Araghchi: Serikali mpya ya Iran ina azma ya kuimarisha uhusiano na Afrika
Waziri mpya wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi amesema kuwa kipaumbele cha kwanza katika sera za kigeni ni nchi jirani na kipaumbele cha pili ni kupanua uhusiano na Afrika na Asia Mashariki. Ameongeza kuwa kipaumbele cha tatu ni nchi zilizosimama upande wa Iran katika hali ngumu.
Araghchi ameyasema hayo katika mahojiano ya televisheni siku ya Ijumaa, siku mbili baada ya kuidhinishwa na bunge kama waziri mpya wa mambo ya nje wa Iran.
Araghchi amesema serikali imepewa maagizo na Kiongozi Muadhamu kuhusu kusambaratisha vikwazo vilivyowekwa dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu na kuhakikisha vikwazo hivyo haramu haviathiri maisha ya wananchi.
Ameendelea kusema kuwa sera ya kigeni ya serikali inalenga kuwa na ushiriki amilifu kwenye vikao vya kimataifa ili kulinda maslahi ya taifa, eneo na ulimwengu wa Kiislamu.
Wakati huo huo, katika mazungumzo ya simu na mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell siku ya Alhamisi, Araghchi pia alibadilishana mawazo kuhusu mazungumzo ya kuondoa vikwazo dhidi ya Iran.
Awali, Araghchi alitangaza nia ya Iran ya kudhibiti mivutano na Marekani na kurejesha uhusiano bora na nchi za Ulaya, kwa sharti kuwa zisitishe uadui wao dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.
Araqchi pia Ijumaa alifanya mazungumzo na mawaziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza na Ufaransa na kuwafahamisha bayana kwamba Iran inahifadhi haki ya kuuadhibu utawala wa Israel kwa jinai yake isiyosameheka ya kumuua kiongozi mkuu wa kisiasa wa Hamas Ismail Haniyeh mwezi uliopita.