Iran yakaribisha kustawisha uhusiano na Ulaya katika anga ya kuheshimiana
Sayyid Abbas Araqchi Waziri wa Mambo ya Nje ya serikali ya 14 ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema katika mazungumzo ya simu na Josep Borrell mwakilishi wa ngazi ya juu wa Umoja wa Ulaya katika masuala ya usalama na sera za je kwamba: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inakaribisha na kuunga mkono kustaiwsha uhusiano na Umoja wa Ulaya katika mazingira ya kuheshimiana pande mbili.
Uhusiano wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Umoja wa Ulaya siku zote umekuwa ukiambatana na changamoto za hapa na pale. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa nyakati tofauti imeunga mkono kustawisha uhusiano na Umoja wa Ulaya na pia na nchi za Ulaya hata hivyo Ulaya haijaonyesha nia yake njema yakustaiwsha uhusiano na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na suala hili limeathiri pakubwa uhusiano wa pande mbili. Suala hili pia lilipamba moto baada ya mwaka 2018 wakati Donald Trump alipoiondoa kinyume cha sheria Marekani katika mapatano ya nyuklia ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kundi la nchi za 5+1 maarufu kama JCPOA. Umoja wa Ulaya pia ingawa ulilaani hatua hiyo ya Trump ya kujitoa kwa upande mmoja katika makubaliano ya JCPOA lakini haikuchukua hatua yoyote ya kulinda maslahi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa mujibu wa JCPOA.
Kwa kuzingatia hilo, viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran akiwemo Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu walisisitiza mara kadhaa kuwa ingawa Iran inakaribisha kustawisha uhusiano na Umoja wa Ulaya na nchi za Ulaya, lakini hilo halikadhibishi kutoridhishwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na hatua na mienendo isiyo ya kirafiki ya Umoja wa Ulaya na pia Iran haina imani na nchi za Ulaya. Kwa sababu hiyo inaonekana kuwa kadhia muhimu zaidi katika uhusiano kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Umoja wa Ulaya na pia na baadhi ya nchi za Ulaya ni kule kutokuwepo hali ya kuaminiana katika uhusiano na hasa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuuamini Umoja wa Ulaya na baadhi za nchi za Ulaya.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaamini kuwa Umoja wa Ulaya unataka kutekeleza kivitendo sera za kiadui na kiuhasama za Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika uhusiano kati yake na Tehran. Kwa hakika ijapokuwa Umoja wa Ulaya unajaribu kusisitiza kuwa uko tayari kustawisha uhusiano na Jamhuri ya Kiislamu lakini kivitendo hauonekani kuwa na nia njema na hautekelezi hatua zozote kivitendo katika uwanja huo na iko chini ya sera za kiuhasama za Washington.
Serikali ya 14 ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa mara nyingine tena inasisitiza kustawisha uhusiano na Ulaya na wakati huo huo viongozi wa serikali ya 14 akiwemo Rais na Waziri wa Mambo ya Nje wanaamini kuwa kuna ulazima Umoja wa Ulaya kutekeleza kivitendo baadhi ya hatua ili kudhamini maslahi na matakwa ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Jambo hili pia limetiliwa mkazo katika mazungumzo ya simu kati ya Borrell na Araqchi.
Katika mazungumzo ya simu na Sayyid Abbas Araqchi, Josep Borrell sambamba na kumpongeza Ataqchi kwa kuchaguliwa kuwa Waziri Mpya wa Mambo ya Nje wa Iran alisema anatumai kuwa mazungumzo na mashauriano ya kisiasa kati ya Iran na Umoja wa Ulaya yataendelea na kupanuka katika serikali mpya. Sayyid Abbas Araqchi Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia ameashiria nyuga mbalimbali na nyingi za ushirikiano kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Umoja wa Ulaya na kusema: Iran inakaribisha kustaiwsha uhusiano na Umoja wa Ulaya katika anga ya kuheshimiana pande mbili; na kuna umuhimu wa kufanyika mazungumzo ili kutatua matatizo ya pande mbili na kurekebisha sera zisizofaa za nchi za Ulaya.