Kiongozi Muadhamu: Vita baina ya haki na batili kamwe havitakoma
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i115622-kiongozi_muadhamu_vita_baina_ya_haki_na_batili_kamwe_havitakoma
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kisilamu amesema mbele ya wanafunzi wa vyuo vikuu katika maombolezo ya Arubaini ya Imam Husain AS kwamba mapambano baina ya kambi ya Imam Husain na kambi ya Yazid (baina ya haki na batili) kamwe havitomalizika.
(last modified 2026-05-06T11:35:21+00:00 )
Aug 25, 2024 06:56 UTC
  • Kiongozi Muadhamu: Vita baina ya haki na batili kamwe havitakoma

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kisilamu amesema mbele ya wanafunzi wa vyuo vikuu katika maombolezo ya Arubaini ya Imam Husain AS kwamba mapambano baina ya kambi ya Imam Husain na kambi ya Yazid (baina ya haki na batili) kamwe havitomalizika.

Kwa mujibu wa shirika la habari la FARS, ujumbe mbalimbali wa wanachuo kutoka kona zote za Iran, leo asubuhi wameonana na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu hapa Tehran katika maombolezo ya Arubaini ya Imam Husain AS. 

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amesema kuwa, kwenye ziara ya 'Ashura huwa tunasoma maneno yafuatayo: Mimi namwacha salama anayekuacheni salama na ninapigana vita na anayekupigeni vita, hivyo vita baina ya kambi ya Imam Husain AS na kambi ya Yazid kamwe haviwezi kumalizika (kwani ni vita baina ya haki na batili). 

 

Vile vile amewashukuru vijana hao wa vyuo vikuu kwa kuendesha kumbukumbu hizo za Arubaini ya Imam Husain AS kwa njia bora akisema kuwa, Qur'ani imesomwa kwa namna nzuri kabisa, mashairi na Ziara ya Arubaini pia vimesomwa vizuri sana na kuongeza kuwa, mapambano haya baina ya haki na batili yataendelea.

Amekumbusha kuwa, katika safari yake ya kuelekea Karbala, Imam Husain AS alisema mara chungu nzima kwamba, hakutoka ila kwa ajili ya kupambana na dhulma, yaani ni vita vya kupigania haki dhidi ya batili, na vita baina ya kambi hizo mbili haviwezi kumalizika. 

Pia Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kisilamu amewaambia vijana hao wa vyuo vikuu kwamba ni wajibu waelewe jukumu lao na waisake na kuitafuta njia ya kutekeleza vizuri jukumu lao. Amesema, kukusanya mali na fedha hakupaswi kuwa ndilo lengo la maisha yao. Fedha, cheo, nguvu na nafasi ndani ya jamii ni vitu dhalili zaidi kufanywa kuwa ndilo lengo kuu la maisha ya mwanadamu.