Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu: Uzalishaji ndio ufunguo wa matatizo ya kiuchumi
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i115708-kiongozi_wa_mapinduzi_ya_kiislamu_uzalishaji_ndio_ufunguo_wa_matatizo_ya_kiuchumi
Katika kikao chake cha kwanza na Rais na Serikali ya Awamu ya 14, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameeleza mambo muhimu kama vile kuzingatia vipaumbele vya haraka kama mfumuko wa bei na ughali wa bidhaa, ulazima wa kuwepo utawala wa sheria katika masuala ya mtandao na kuzingatia uzalishaji kuwa ndiyo ufunguo wa matatizo ya kiuchumi.
(last modified 2024-08-27T08:49:44+00:00 )
Aug 27, 2024 08:49 UTC
  • Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu: Uzalishaji ndio ufunguo wa matatizo ya kiuchumi

Katika kikao chake cha kwanza na Rais na Serikali ya Awamu ya 14, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameeleza mambo muhimu kama vile kuzingatia vipaumbele vya haraka kama mfumuko wa bei na ughali wa bidhaa, ulazima wa kuwepo utawala wa sheria katika masuala ya mtandao na kuzingatia uzalishaji kuwa ndiyo ufunguo wa matatizo ya kiuchumi.

Ayatullah Ali Khamenei amepongeza na kuenzi harakati tukufu ya wananchi katika Siku ya Arubaini ya Imam Hussein (as) na kuipongeza Wiki ya Serikali, na ameitaja fursa ya kuwatumikia wananchi na kufanya jitihada za maendeleo ya nchi kuwa ni neema kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Ameongeza kwa kusema: Thaminini amana hii ya Mwenyezi Mungu na wananchi, na eleweni kwamba fursa ya miaka 4 ya kuhudumia taifa inapita kwa kasi ya umeme na upepo; lakini, mambo makubwa yanaweza pia kufanywa katika kipindi hicho.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema taifa la Iran lina uwezo wa kutengeneza watu wenye vipaji vikubwa. Ameashiria watu mashuhuri kama Khaja Nasiruddin Tusi, Ibn Sina, Mulla Sadra na Zakaria Razi na akasema: Hizi ni nembo za uwezo wa kifikra usio na kikomo wa taifa la Iran, na hivi sasa pia inawezekana kutengeneza watu wenye vipaji kutokana na vijana wenye uwezo hapa nchini. 

Ayatullah Khamenei

Ametaja uwezo wa kisiasa wa Iran na kina cha kistratijia kuwa ni nguvu za kieneo na kuongeza kuwa: Uzoefu chanya na hasi wa miaka 45 iliyopita ni miongoni mwa nukta zenye thamani kubwa zinazopaswa kutiliwa maanani.

Vilevile ametaja nishati ya nyuklia kama mojawapo ya vipaumbele vya kimiundombinu na muhimu kwa mustakabali wa nchi. Amekosoa matamshi hasi yanayohoji faida za nishati ya nyuklia hapa nchini na kusema: Nchi haiwezi kujinyima suala la kisayansi, kiufundi na la kimaendeleo duniani na kuanza kulifuatilia tena baada ya kubakia nyuma kwa miaka mingi.

Amesisitiza kuwa ufunguo wa kutatua matatizo ya kiuchumi ya nchi ni uzalishaji na uimarishaji wa sekta hiyo na kusema: Matatizo ya mfumuko wa bei, ajira na thamani ya sarafu ya taifa yatatatuliwa kwa kuimarisha na kutilia maanani suala la uzalishaji.

Kiongozi Muadhamu na Rais Pezeshkian

Akieleza jinsi Rais alivyoshauriana naye kuhusu baraza la mawaziri, Ayatullah Ali Khamenei amesema: Nilipasisha baadhi ya majina ya watu ambao nawajua au nilikuwa na uhakika juu ya sifa zao kutoka vyanzo vya kuaminika, na nilitilia mkazo baadhi ya majina; lakini kuhusu idadi kubwa ya wale ambao siwajui nilisema kuwa sina maoni kuhusiana nao; na Rais ameweza kulishawishi Bunge na kupata kura ya imani kwa mawaziri wake wote.