Iran: Utawala wa Israel ni kikwazo kikubwa kwa amani na chanzo cha mivutano katika eneo
Abbas Araghchi Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameukosoa vikali utawala ghasibu wa Israel na kusema ukatili wake usiokoma kuwa ndio sababu kuu ya kuongezeka hali ya wasiwasi na migogoro katika eneo la Asia Magharibi.
Mwanadiplomasia huyo mkuu wa Iran aliyasema hayo wakati wa mazungumzo ya simu na mwenzake wa Jordan Ayman Safadi siku ya Ijumaa. Matamshi hayo yamehusu vita vya mauaji ya kimbari ambayo yamekuwa yakitekelezwa na utawala katili wa Israeli katika Ukanda wa Gaza tokea Oktoba mwaka jana na hali kadhlika hujuma mpya za utawala huo katika eneo la Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu, pamoja na kushadidi chokochoko za utawala huo dhidi ya Lebanon, na mauaji ya kigaidi ya viongozi wakuu wa muqawama katika eneo.
Kama mfano, Araghchi amesema utawala huo wa Israel ni kikwazo kikubwa zaidi katika makubaliano ya usitishaji vita dhidi ya Gaza. Katika vita hivyo vya mauaji ya kimbari, utawala katili wa Israel hadi sasa umeua zaidi ya Wapalestina 40,600, wengi wao wakiwa wanawake na watoto.
Araghchi amesema, "Jamhuri ya Kiislamu itaunga mkono makubaliano [ya mapatano] ambayo yanakidhi mahitaji ya watu wa Palestina na muqawama."
Amesisitiza haja ya kuchukuliwa hatua madhubuti na jumuiya ya kimataifa katika kukomesha mauaji hayo ya kimbari na kuwezesha kufikishwa misaada ya kibinadamu Gaza.
Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jordan amesema, "Ni muhimu kusitishwe mashambulizi dhidi Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi haraka iwezekanavyo."