Azma ya Iran na Russia ya kukamilisha hati jumuishi ya ushirikiano
Akikaribisha matamshi ya Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusu kuendelea uhusiano na Russia, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Russia amesema: Hati ya makubaliano jumuishi ya ushirikiano kati ya tehran na Moscow itakamilika katika siku chache za usoni.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Russia, zikiwa nchi mbili jirani, daima zimekuwa zikielekea katika kustawisha uhusiano wa pande mbili na vilevile kupanua ushirikiano wa kieneo. Katika muongo uliopita na baada ya mgogoro wa Syria, uhusiano kati ya Iran na Russia umeimarika zaidi. Tehran na Moscow zilishirikiana kwa karibu katika mapambano dhidi ya ugaidi hususan nchini Syria. Ushirikiano huu kwa kiasi kikubwa chimbuko lake ni uelewa wa pamoja na vitisho vya pamoja vinavyozikabili pande hizi mbili. Aidha, Tehran na Moscow zimeelekea kwenye ushirikiano wa karibu na kukamilisha makubaliano ya ushirikiano wa muda mfupi na mrefu katika uwanja wa uhusiano wa pande mbili.
Jamhuri ya Kiislamu na Russia zilitiliana saini makubaliano ya kimkakati ya miaka 20 mnamo 2001, ambayo yaliongezewa muda miaka mingine 5 mnamo 2020. Pande hizo mbili pia zilikubaliana mnamo 2020 kuandika waraka mpya kuchukua nafasi ya ule wa awali. Uhusiano wa nchi hizi mbili hususan katika kipindi cha serikali ya awamu ya 13 ya Iran ulichukua mkondo wa kasi zaidi. Kwa kuapishwa kwa serikali ya 14 inayoongozwa na Daktari Masoud Pezeshkin, Rais huyu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alisisitiza kuendelezwa uhusiano wa taifa hili na Russia.
Baada ya kushinda uchaguzi wa rais, Masoud Pezeshkian alisisitiza katika mazungumzo ya simu na Rais Vladmir Putin wa Russia juu ya ufuatiliaji na utekelezwaji wa makubaliano yaliyofikiwa kati ya nchi hizo mbili katika kipindi cha uongozi wa Shahid Ebrahim Raisi na kusema: Tehran iko tayari kutia saini mkataba mpya wa makubaliano na Moscow wakati wa mkutano wa nchi za Jumuiya ya Kiuchumi ya BRICS, ambao umepangwa kufanyika katika mji wa Kazan, Russia mwezi ujao wa Oktoba.
Matamshi haya ya Rais Pezeshkian yalikaribishwa kwa mikono miwili na Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Russia. Sergey Lavrov amesema kuwa, matamshi ya Rais Pezeshkian kuhusiana na kudumishwa kwa uhusiano wa Tehran na Moscow yanaonyesha msimamo wa uaminifu wa rais mpya wa Iran. Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Russia pia amebainisha kuwa, uhusiano kati ya Russia na Iran unaendelea kwa kasi, na idadi kubwa ya miradi ya pande mbili hivi sasa imo katika hatua ya kutekelezwa.
Hivi karibuni Andrey Rudenko, Naibu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Russia alisema kuwa, kuhaririwa hati mpya ya mapatano ya Iran na Russia yenye lengo la kuboresha hali ya uhusiano kati ya nchi hizi mbili hadi kufikia kiwango cha ushirikiano wa kistratijia na wa kina kumechukua karibu miaka miwili na nusu, na leo inaweza kutambuliwa kuwa imekamilika.
Azma ya Tehran na Moscow ya kupanua uhusiano iko katika hali ambayo uhusiano kati ya nchi hizo mbili unakabiliwa na upinzani mkubwa katika ngazi ya kimataifa. Madola ya Magharibi hususan dola la kibeberu la Marekani yamekuwa yakieleza mara kwa mara upinzani wao wa kustawishwa uhusiano kati ya Iran na Russia na pia yameweka vikwazo vingi katika njia ya kustawishwa uhusiano kati ya Moscow na Tehran ili kuzuia kuweko ushirikiano wa karibu kati ya mataifa haya mawili rafiki.
Hata hivyo, njama hizo zimegonga ukuta na hazijawa na taathira katika uhusiano kati ya nchi hizi mbili na hata mabadiliko ya serikali za Iran nayo hayajawa sababu ya kusita au kusimama harakati na mwendo wa kuimarika kwa uhusiano wa pande mbili kati ya Moscow na Tehran.