Marais wa Iran na Iraq wakutana Baghdad na kusisitiza kuimarisha uhusiano
Marais wa Iran na Iraq wamesisitiza juu ya kupanuliwa ushirikiano wa pande mbili katika nyanja mbalimbali za kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni na juhudi za pamoja za kuhimiza uthabiti katika eneo hili.
Katika kikao na Abdul Latif Jamal Rashid, Rais wa Iraq, Rais Masoud Pezeshkian wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza ulazima wa kutiliwa maanani zaidi ushirikiano wa pande mbili na wa kieneo.
Rais wa Iran ametoa wito wa kuanzishwa kwa tume za wataalamu kati ya nchi hizo mbili ili kupanua uhusiano wa kisiasa, kiuchumi, kiutamaduni na kijamii kadiri inavyowezekana.
Rais Pezeshkian pia ameashiria historia ndefu ya nchi mbili za Iran na Iraq na kusisitiza ulazima wa kuundwa umoja wa pamoja wa nchi za Kiislamu.
Halikadhalika amesesitiza kuhusu kuanzishwa mchakato wa kuondoa mipaka ya nchi za Kiislamu, kama ilivyo katikak nchi za Umoja wa Ulaya.
Rais wa Iran amesema kuimarishwa umoja baina ya nchi za Kiislamu kutasambaratisha vikwazo na kuongeza kuwa: "Umoja kati ya nchi za Kiislamu ndio utakuwa ufunguo wa kung'oa mizizi ya ugaidi wa Kizayuni."

Katika kikao hicho Rais wa Iraq sanjari na kumkaribisha Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amemuenzi hayati Rais wa Iran Shahidi Ebrahim Raisi na waziri wake wa mambo ya nje Hossein Amir Abdollahian.
Abdul Latif Jamal Rashid amesisitiza hatua ya kuiondoa sarafu ya dola ya Marekani kwenye miamala ya kifedha.
Halikadhalika amekaribisha kuundwa kwa makubaliano na kutiwa saini hati zaidi za ushirikiano kati ya nchi mbili za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Iraq.
Rais Masoud Pezeshkian wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliwasili mjini Baghdad leo asubuhi kwa lengo la kukutana na kushauriana na viongozi wa nchi jirani ya Iraq kwa lengo la kupanua na kuimarisha uhusiano kati ya nchi mbili hizi za Kiislamu.