Iran yataka Baraza la Usalama lilaani mashambulizi ya kigaidi nchini
Iran imelitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilaani shambulio la kigaidi katika mkoa wake wa Sistan na Baluchestan.
Amir Saeed Iravani, Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa siku ya Ijumaa aliliandikia Baraza la Usalama kutaka hatua zinazofaa zichukuliwe dhidi ya wahusika wa shambulio hilo kusini mashariki mwa Iran.
Iravani pia amesema Tehran itahakikisha wahusika wa ugaidi huo wanafikishwa kwenye vyombo vya sheria ili waadhibiwe.
Iravani ameongeza kuwa kitendo hicho cha kigaidi kimepelekea kuuawa shahidi maafisa watatu wa usalama ambao ni Mohammad Amin Narouei, Parsa Soozani na Amir Ebrahimzadeh.
Maafisa hao watatu wa kikosi cha kulinda mpaka waliuawa wakati watu wenye silaha walipofyatua risasi kwenye kituo cha mafuta katika mji wa Mirjaveh. Kundi la kigaidi linalojiita Jaish al-Adl limedai kuhusika na tukio hilo. Kundi hilo limetekeleza mashambulizi kadhaa ya kigaidi katika mkoa wa Sistan na Baluchestan.
Katika barua yake kwa Baraza la Usalama, Iravani amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inalaani vikali ugaidi huo wa kutisha na inasisitiza dhamira yake isiyoyumba ya kuhakikisha kwamba waliohusika wanafikishwa mbele ya sheria na kuwajibishwa.
Jaish al-Adl ni kundi la kigaidi lenye makao yake makuu nchini Pakistani ambalo limehusika katika mashambulizi mengi ya kigaidi dhidi ya Iran.
Iran mara kadhaa imeitaka Pakistan kuzuia makundi ya kigaidi kujikita katika eneo la mpakani.