Mkutano wa 38 wa Umoja wa Kiislamu kuanza Alkhamisi hii Tehran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i116374-mkutano_wa_38_wa_umoja_wa_kiislamu_kuanza_alkhamisi_hii_tehran
Kongamano la 38 la Umoja wa Kiislamu litafanyika Tehran kuanzia Alkhamisi ijayo likiwa na kauli mbiu ya "Ushirikiano wa Kiislamu ili kufikia tahamani za pamoja kwa kutilia mkazo suala la Palestina".
(last modified 2026-02-05T09:20:29+00:00 )
Sep 15, 2024 00:21 UTC
  • Mkutano wa 38 wa Umoja wa Kiislamu kuanza Alkhamisi hii Tehran

Kongamano la 38 la Umoja wa Kiislamu litafanyika Tehran kuanzia Alkhamisi ijayo likiwa na kauli mbiu ya "Ushirikiano wa Kiislamu ili kufikia tahamani za pamoja kwa kutilia mkazo suala la Palestina".

Hayo yameelezwa na Sheikh Hamid Shahriari, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Pamoja Madhehebu za Kiislamu alipokuwa akifafanua mipango ya mkutano huo. Shahriari ameashiria kujiepusha na chuki za kikabila na kikaumu na kuepuka vita na akasema: Thamani hizi zitatiliwa mkazo katika Kongamano la Umoja wa Kiislamu mwaka huu.

Akielezea sababu ya kuchagua kaulimbiu ya mkutano huu amesema: Tunataka ushirikiano baina ya nchi za Kiislamu uonekane pia kivitendo na ulete mafungamano zaidi baina ya nchi za Kiislamu.

Vikao vya utangulizi wa mkutano huo vilianza jana.

Shahriari amesema: Sherehe ya ufunguzi wa mkutano huo itafanyika siku ya Alkhamisi kwa kuhudhuuriwa na Rais Masoud Pezeshkian wa Jamahuri ya Kiislamu ya Iran katika ukumbi wa mikutano ya Kiislamu mjini Tehran.

Mkutano wa mwaka jana (2023) wa Umoja wa Kiislamu

 

Ikumbukwe kuwa Mkutano wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu Iran hufanyika kila mwaka hapa hapa Iran katika siku za kuadhimisha Maulid ya Mtume Muhammad al Mustafa SAW, siku ambazo ni maarufu kama siku za Maulidi. Waislamu wa madhehebu ya Sunni wanaadhimisha siku hiyo tarehe 12 Rabiul Awwal na Waislamu wa Madhehebu ya Shia wanamini siku hiyo ni tarehe 17 Rabiul Awwal.

Hayati Imam Khomeini MA, Kiongozi mwanzilishi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, ambaye binafsi alikuwa mstari wa mbele kulingania umoja wa Kiislamu alikitangaza kipindi cha muda uliopo baina ya tarehe hizo mbili kiwe ni "Wiki ya Umoja wa Waislamu" kwa lengo la kuimarisha mashikamano na udugu baina ya madhehebu za Kiislamu.