Tehran na Moscow zasisitiza kufikia makubaliano jumuishi ya kimkakati kati yao
Rais Vladimir Putin wa Russia amekubali pendekezo la Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo ya kutiwa saini makubaliano ya kina ya ushirikiano wa kimkakati na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Rais Putin ametoa amri na kukubali pendekezo la Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo, ambalo lilikubaliwa na mashirika ya serikali ya shirikisho lenye nia ya kusainiwa makubaliano ya kina ya ushirikiano wa kimkakati kati ya Shirikisho la Russia na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Katika mkutano wa mwisho kati ya maafisa wa Tehran na Moscow, Rais Masoud Pezeshkian wa Jamhuri ya Iran, siku ya Jumanne wakati alipokutana na Sergei Shoigu, Katibu wa Baraza la Usalama la Russia hapa mjini Tehran, aliashiria rekodi chanya ya uhusiano mzuri uliopo kati ya nchi mbili na kusisitiza kuwa serikali ya 14 ya Iran itafuatilia kwa karibu ushirikiano na hatua zilizochukuliwa kwa ajili ya kuimarisha mahusiano ya mataifa haya mawili.
Tarehe 12 mwezi Septemba, Rais Vladmir Putin wa Russia katika kikao na Ali Akbar Ahmadian, Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kando ya kikao cha maafisa wa ngazi za juu wa usalama wa nchi wanachama wa BRICS huko St. Petersburg alisema kuwa serikali ya Russia inaunga mkono njia za usafiri na mawasiliano za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Katika miaka ya hivi karibuni, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Russia zimekuwa na ushirikiano mkubwa katika njia ya kuimarisha uhusiano wa pande mbili katika sekta mbalimbali zikiwemo za kiuchumi, kisiasa, kijeshi na kiusalama ambapo mchakato wa ushirikiano huo unaendelea kuimarika siku hadi siku.