Usafirishaji nje bidhaa waanza tena kwenye Bandari ya Shahid Rajaee baada ya mlipuko wa jana
(last modified Sun, 27 Apr 2025 11:57:18 GMT )
Apr 27, 2025 11:57 UTC
  • Usafirishaji nje bidhaa waanza tena kwenye Bandari ya Shahid Rajaee baada ya mlipuko wa jana

Idara ya Forodha ya Irani imetangaza kuwa: Taratibu za forodha za usafirishaji na uagizaji wa bidhaa kutoka nje ya nchi zimeanza tena katika Forodha ya Bandari ya Shahid Rajaee huko Bandar Abbas.

Ni baada ya mripuko mkubwa ulitokea jana katika Bandari ya Shahidi Rajaee kusini mwa Iran na kusababisha uharibifu na hasara mkubwa. Hadi sasa watu 28 wameripotiwa kuaga dunia, sita hawajulikani waliko na wengine 800 wamejeruhiwa. Sababu halisi ya mlipuko huo bado haijajulikana. 

Taarifa ya Idara ya Forodha ya Iran imesema, shughuli na taratibu za forodha zimeanza tena leo Jumapili.

Serikali ya Iran imetangaza siku ya kesho Jumatatu, kuwa ni siku ya maombolezo ya kitaifa kufutia maafa yaliyosababishwa na mlipuko huo.

Vilevile mkoa wa Hormozgan, kusini mwa Iran, umetangaza siku tatu za maombolezo ya umma kutokana na mlipuko mbaya uliotokea kwenye Bandari hiyo ya Shahid Rajaee. Bandari hiyo yenye eneo la hekta zipatazo 2,400, iko katika mji wa Bandar Abbas, na inashughulikia tani milioni 80 za bidhaa kwa mwaka.

Mkuu wa Shirika la Hilali Nyekundu la Iran (IRCS) Pirhossein Koolivand amesema kuwa majeruhi 190 bado wanaendelea kupata matibabu.