Iran yaapa kujibu kwa "njia muafaka" maamuzi haribifu ya Bodi ya IAEA
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i127448
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amekosoa vikali hatua ya kichokozi ya Marekani na washirika wake wa Ulaya ya kuwasilisha azimio dhidi ya Iran katika Bodi ya Magavana ya Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA), akionya kuwa uamuzi wowote wa "kutozingatia busara" kutoka kwa wajumbe wa bodi hiyo ya wanachama 35 utajibiwa kwa hatua muafaka kutoka Tehran.
(last modified 2025-06-11T12:58:21+00:00 )
Jun 11, 2025 12:58 UTC
  • Iran yaapa kujibu kwa

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amekosoa vikali hatua ya kichokozi ya Marekani na washirika wake wa Ulaya ya kuwasilisha azimio dhidi ya Iran katika Bodi ya Magavana ya Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA), akionya kuwa uamuzi wowote wa "kutozingatia busara" kutoka kwa wajumbe wa bodi hiyo ya wanachama 35 utajibiwa kwa hatua muafaka kutoka Tehran.

Abbas Araghchi alitoa tahadhari hiyo katika mazungumzo ya simu na mwenzake wa Japan, Takeshi Iwaya, siku ya Jumanne, walipokuwa wakijadili masuala mbalimbali ya uhusiano wa pande mbili, kieneo na kimataifa.

Akiangazia mazungumzo yanayoendelea kati ya Iran na Marekani kuhusu mpango wa nyuklia wa Tehran, Araghchi amesisitiza dhamira ya Iran ya kulinda haki halali na zisizoweza kunyimwa watu wake za kufaidika na nishati ya nyuklia kwa matumizi ya amani, ikiwemo haki ya kurutubisha madini ya urani.

Araghchi pia amekemea hatua ya Marekani na nchi za Ulaya – Ufaransa, Ujerumani na Uingereza – ya kuandaa azimio dhidi ya Iran katika Bodi ya Magavana ya IAEA, wakati mazungumzo ya nyuklia yasiyo ya moja kwa moja kati ya Tehran na Washington yakiendelea.

"Uamuzi wowote usio wa busara na wa kuharibu kutoka kwa Bodi ya Magavana dhidi ya Iran utajibiwa kwa hatua inayofaa kutoka upande wetu, na mzigo wa matokeo yake bila shaka utabebwa na wale wanaolitumia vibaya shirika hili kwa maslahi ya kisiasa," amesema Waziri huyo wa Mambo ya Nje wa Iran.

Araghchi amesema kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inafuata msimamo wa msingi, unaotokana na mafundisho ya Kiislamu, wa kutojihusisha na uundaji wa silaha za nyuklia, lakini akaongeza: "Hatutakubali kamwe kunyimwa haki ya taifa la Iran ya kutumia nishati ya nyuklia kwa madhumuni ya amani."

Akilisifu taifa la Japan kwa msimamo wake wa usawa katika sera zake za nje, Araghchi amesema: "Tunatumai kuona msimamo na hatua inayofaa kutoka kwa Japan na nchi nyingine wanachama wa Bodi ya Magavana ili kuimarisha njia ya mazungumzo na ushirikiano."

Kwa upande wake, Waziri Iwaya amekaribisha kuendelea kwa mazungumzo kati ya Iran na Marekani, akisisitiza kuwa Iran ina haki ya msingi ya kutumia nishati ya nyuklia kwa shughuli za amani.

Kwa mujibu wa ripoti yake ya hivi karibuni, Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA) limedai kuwa Iran imeongeza kwa kasi akiba yake ya urani iliyosafishwa hadi kiwango cha asilimia 60, kiwango kinachokaribia asilimia 90 kinachohitajika kwa utengenezaji wa silaha za nyuklia.

Shirika hilo lilieleza kuwa kufikia Mei 17, Iran ilikuwa inamiliki takriban kilo 408.6 za urani iliyosafishwa hadi kiwango cha asilimia 60, ikiwa ni ongezeko la kilo 133.8 ikilinganishwa na ripoti ya awali ya mwezi Februari.

Iran, kwa upande wake, imelaani ripoti hiyo ya shirika la Umoja wa Mataifa linalosimamia masuala ya nyuklia, ikiitaja kuwa ya kisiasa na isiyo na mizani, na kusema kuwa imetungwa kwa mashinikizo kutoka mataifa ya Ulaya.