Rais Pezeshkian aipongeza timu ya astronomia ya Iran kwa kushinda ubingwa wa dunia
Rais Masoud Pezeshkian wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameipongeza Timu ya Olimpiadi ya Astronomia ya Iran kwa kushinda taji la ubingwa wa dunia kwa mwaka wa pili mfululizo.
Timu ya Iran ilishinda ubingwa wa dunia katika toleo la 18 la Olimpiadi ya Kimataifa ya Astronomia na Astrofizikia (IOAA) huko Mumbai, India, ambapo wanafunzi zaidi ya 300 kutoka shule za upili kutoka nchi 64 walishindana. Time ya Iran imeweza kupata medali tano za dhahabu katika mashindano hayo yaliyofanyika Agosti 11 hadi 21 mwaka huu.
Pezeshkian ameipongeza timu hiyo kutokana na mafanikio yao ya ajabu ambayo ni ishara ya kujitolea na juhudi za vijana hawa wenye talanta, ambao wanaendelea kuleta heshima na sifa kwa taifa lao.
Ameongeza kusema, "Ushindi huu unaotia moyo, uliofanikishwa kupitia juhudi za muda wote za vijana wenye vipaji na wanaojenga mustakabali wa nchi hii, ni thibitisho kwamba kizazi chetu kipya kinaweza kung'aa katika nyanja yoyote waliyoiamua na kuinua bendera ya Iran kufikia kilele cha maendeleo na heshima."
Rais Pezeshkian amebaini kuwa, "Bila shaka, mafanikio haya ya thamani ni matokeo ya juhudi zisizoyumba za familia zenye busara za wanafunzi hawa, makocha waliojitolea, na wote walioshiriki katika sekta ya elimu ambao wameunda mazingira ya ukuaji na ustawi kwa kujitolea na hisia za uwajibikaji."
Rais wa Iran ameongeza kuwa serikali yake, ikiwa na imani na uwezo wa vijana, imejizatiti kuunga mkono vipaji vya kipekee na kubadilisha Iran kuwa kituo cha kanda cha elimu na teknolojia."
Olimpadi ya Kimataifa ya Astronomia na Astrofizikia ni mashindano ya kila mwaka kwa wanafunzi wa shule za upili yanayojikita katika astronomia na astrofizikia, na ni sehemu ya Olimpiadi za Sayansi za Kimataifa.
Waliokuwa katika timu ya taifa ya Iran katika mashindano hayo walikuwa Ali Naderi, Hossein Masoumi, Hirbod Foodazi, Arshia Mirshamsi Kakhaki na Hossein Soltani.
Timu ya Iran ilionyesha ufanisi wa kipekee, ikishinda medali zote tano za dhahabu na kushika nafasi ya kwanza katika mashindano hayo ya sayansi ya dunia ya 2025 nchini India.