Iran yaionya E3: Fanyeni chaguo la busara, mkitekeleza 'snapback' ushirikiano na IAEA utasita
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i130102-iran_yaionya_e3_fanyeni_chaguo_la_busara_mkitekeleza_'snapback'_ushirikiano_na_iaea_utasita
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imezionya Uingereza, Ufaransa na Ujerumani kwamba itasitisha maingiliano yake na shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu masuala ya nyuklia iwapo nchi hizo tatu zitalifanya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lirejeshe vikwazo dhidi yake.
(last modified 2025-10-22T06:10:45+00:00 )
Aug 28, 2025 07:11 UTC
  • Iran yaionya E3: Fanyeni chaguo la busara, mkitekeleza 'snapback' ushirikiano na IAEA utasita

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imezionya Uingereza, Ufaransa na Ujerumani kwamba itasitisha maingiliano yake na shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu masuala ya nyuklia iwapo nchi hizo tatu zitalifanya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lirejeshe vikwazo dhidi yake.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Kazem Gharibabadi ameyasema hayo Jumatano baada ya kurejea nchini kutoka katika mazungumzo na wawakilishi wa nchi hizo yaliyofanyika mjini Geneva.

Kwa mujibu wa Gharibabadi, ujumbe wa kidiplomasia wa Iran kwenye mazungumzo hayo "uliweka wazi" kwa pande za Ulaya kwamba ikiwa wataweza kulazimisha kurejeshwa vikwazo hivyo, "Iran itatoa mjibizo unaohitajika."

Troika ya Ulaya inayojumuisha Uingereza, Ufaransa na Ujerumani imekuwa ikijaribu kuwezesha kurejeshwa vikwazo hivyo, kwa madai yasiyo na ushahidi wowote, kwamba Iran ilikiuka makubaliano ya nyuklia ya 2015 kwa "kugeuza" mpango wake wa amani wa nishati ya nyuklia kuwa wenye malengo ya kijeshi.

Ili kuweza kurejesha vikwazo hivyo, nchi hizo tatu kubwa za Ulaya zimekuwa zikishinikiza kutekelezwa utaratibu unaoitwa "snapback" ambao umejumuishwa katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.

Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) hata hivyo, haujapata hadi sasa uthibitisho wowote wa madai ya nchi hizo kwamba Iran imegeuza mkondo wa mpango wake wa nyuklia kuwa na malengo ya kijeshi na hivyo kukiuka makubaliano ya JCPOA.

Gharibabadi amesema troika ya Ulaya imetahadharishwa kuhusu matokeo mabaya ya "kuchagua kupuuza nia njema na mtazamo mzuri wa Jamhuri ya Kiislamu, ambayo imekuwa ikisisitizia utatuzi wa kidiplomasia wa suala hilo."

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amebainisha kwamba, ikiwa nchi hizo zitachukua hatua hiyo, Jamhuri ya Kiislamu itajibu mapigo kwa kusitisha mazungumzo yake na nchi hizo za UIaya.

"Tumesisitiza pia kwamba ikiwa hali hii itatokea, Ulaya itajiweka kando ya mkondo wa kidiplomasia na mazungumzo na Iran", ameongeza Gharibabadi.../