Yemen: Jeshi la Majini la Marekani tumelitimua katika Bahari Nyekundu
(last modified Tue, 10 Sep 2024 11:16:49 GMT )
Sep 10, 2024 11:16 UTC
  • Yemen: Jeshi la Majini la Marekani tumelitimua katika Bahari Nyekundu

Harakati ya mapambano ya Kiislamu ya Ansarullahi ya Yemen imesema kuwa, imefanikiwa kuwatimua wanajeshi wa Marekani katika Bahari Nyekundu.

Shirika la habari la FARS limemnukuu Mohammad Ali al Houthi, mjumbe mwandamizi wa Baraza Kuu la Kisiasa la Yemen akisema hayo leo Jumanne katika mtandao wa kijamii wa Telegram na kuongeza kuwa, baada ya kupita miaka mingi ya kuvamiwa na kuzingirwa kila upande, hatimaye kwa taufiki wa Allah, taifa la Yemen limeweza kupiga hatua na kupata mafanikio makubwa katika nyuga tofauti.

Ameongeza kuwa, mafanikio ya karibuni kabisa liliyopata taifa la Yemen ni kuwatimua wanajeshi wa Marekani katika Bahari ya Sham (Bahari Nyekunduu).

Vilevile amesema: Tunawatangazia wazi maadui kwamba, kama wanaweza kuweka dau la kushindana nasi, basi waelewe kuwa taifa la Yemen lina hamu kubwa ya kuweka dau hilo na kama watataka tuwekeane masharti kwenye wakati na muda maalumu, sisi pia tuko tayari kwa ajili ya kutoa vipigo zaidi kwa maadui, kwa idhini ya Mwenyezi Mungu.

Katika kipindi cha miezi ya hivi karibuni, jeshi la Yemen na vikosi vya kujitolea vya wananchi wa nchi hiyo vimepiga meli kadhaa za kijeshi za Marekani ikiwa ni sehemu ya kuwaunga mkono wananchi wa Palestina wanaofanyiwa jinai kubwa na utawala wa Kizayuni kwa uungaji mkono kamili wa Marekani na madola mengine ya kibeberu.

Vikosi vya Ulinzi vya Yemen vimefunga njia zote za Bahari Nyekundu kuzuia vyombo vya Israel, Marekani na kila chombo cha baharini kisipeleke chochote kwa utawala wa Kizayuni, hatua ambayo inaendelea kuisababishia hasara kubwa Israel.