Hizbullah yashambulia Tel Aviv kwa makombora ya balestiki
Harakati ya Muqawama ya Hizbullah ya Lebanon inaendelea kutumia mkakati wake wa kujihami wa "Moto Kwa Moto, Beirut kwa Tel Aviv" katika kukabiliana na hujuma za kinyama za utawala katili wa Israel dhidi ya Lebanon.
Siku ya Jumatatu, harakati hiyo ilishambulia mara kadhaa jiji la Tel Aviv katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na kusisitiza kwamba haitalegeza kamba hata kama utawala wa Kizayuni wa Israel utaendeleza mashambulizi yake makali dhidi ya raia wa Lebanon.
Taarifa zinasema Hizbullah imevurumisha makombora kadhaa ya balestiki, yasiyopungua manne, na pia imetumia ndege za kivita zisizo na rubani katika mashambulizi hayo ambayo yanaripotiwa kusababisha maafa makubwa. Utawala wa Kizayuni wa Israel kwa kawaida huficha idadi ya waliouawa ili kuzuia Wazayuni kuingiwa na hofu zaidi na kuhama ardhi zinazokaliwa kwa mabavu ambazo zimepachikwa jina la Israel.
Kwa mujibu wa Kanali ya 12 ya utawala huo, taswira za video zilizosambaa mitandaoni zinaonyesha mifumo ya makombora ya Israel ikishindwa kunasa moja ya makombora ambayo yamesababisha hasara za moja kwa moja karibu na maduka makubwa mjini humo.
Vyanzo vya polisi ya Israel vimethibitisha kwamba operesheni hiyo imesababisha "pigo la moja kwa moja," na kuongeza kwamba, "kuna hofu ya kuanguka majengo."
Video inayoonesha mfungo wa ulinzi wa anga wa Israel ukishindwa kukabiliana na kombora la Hizbullah
Taarifa zinasema Waisraeli wamepoteza maisha katika mji wa Ramat Gan, mashariki mwa Tel Aviv, baada ya milipuko minne kusikika katika eneo lililolengwa.
Hizbullah imekuwa ikiendesha mamia ya oparesheni za kijeshi dhidi ya upande wa kaskazini wa ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu (Israel) tangu mwezi Oktoba mwaka jana, wakati utawala huo ghasibu ulipoanza kuanzisha vita vya mauaji ya kimbari dhidi ya Gaza sambamba na kuishambulia Lebanon mara kwa mara hasa katika kipindi cha miezi miwili iliyopita.
Mashambulizi ya kikatili ya utawala haramu wa Israel yamepelekea zaidi ya Wapalestina 44,000 kupoteza maisha tokea Oktoba mwaka jana, wengi wao wakiwa wanawake na watoto. Aidha katika kipindi cha miezi miwili Israel imeua takribani Walebanoni 3,510. Hizbullah imeapa kulipiza kisasi damu ya mashahidi hao Wapalestina na Walebanon.