Ukidhabi mkubwa wa Israel kuhusu mashambulizi yake dhidi ya hospitali za Ghaza wafichuka
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i126444-ukidhabi_mkubwa_wa_israel_kuhusu_mashambulizi_yake_dhidi_ya_hospitali_za_ghaza_wafichuka
Gazeti moja la lugha ya Kiebrania limefichua kwamba jeshi la Israel lilitoa taarifa za uongo kuhusu kuwepo handaki la Hamas chini ya "Hospitali ya Ulaya" (The European Hospital) huko Khan Yunis, kusini mwa Ukanda wa Ghaza, na kwamba hospitali hiyo ililengwa na mashambulizi makubwa ya mabomu mara mbili ndani ya saa 24 bila ya kuweko handaki lolote la HAMAS.
(last modified 2025-05-16T02:20:12+00:00 )
May 16, 2025 02:20 UTC
  • Ukidhabi mkubwa wa Israel kuhusu mashambulizi yake dhidi ya hospitali za Ghaza wafichuka

Gazeti moja la lugha ya Kiebrania limefichua kwamba jeshi la Israel lilitoa taarifa za uongo kuhusu kuwepo handaki la Hamas chini ya "Hospitali ya Ulaya" (The European Hospital) huko Khan Yunis, kusini mwa Ukanda wa Ghaza, na kwamba hospitali hiyo ililengwa na mashambulizi makubwa ya mabomu mara mbili ndani ya saa 24 bila ya kuweko handaki lolote la HAMAS.

Gazeti la Kizayuni la Haaretz limefichua kwamba: "Hakuna handaki la HAMAS ndani ya hospitali hiyo, kinyume na madai ya jeshi la Israel, na hakuna ushahidi wa kuunga mkono madai kwamba kuna handaki limepita chini ya kituo hicho cha matibabu."

Kwa mujibu wa taarifa za Wizara ya Afya na Ulinzi wa Raia ya Ghaza, jeshi la Israel lilifanya mauaji ya kutisha Jumanne jioni kwa mashambulizi makali ya anga dhidi ya Hospitali ya Ulaya kusini mwa Ghaza na kuua shahidi Wapalestina 34 na kujeruhi wengine wengi.

Baadhi ya vyombo vya habari vya Kizayuni viliripoti kwamba lengo la shambulio hilo la kijinai la Israel lilikuwa ni kumuua kigaidi, Muhammad Sinwar, kiongozi mashuhuri wa Brigedi za Qassam, tawi la kijeshi la Hamas ambaye ni ndugu wa shujaa maarufu wa Muqawama wa Palestina, Yahya Sinwar aliyeuawa shahidi tarehe 16 Oktoba 2024 akiwa mstari wa mbele wa mapambano kuthibitisha kwamba hakuwa mtu mwoga wa kujificha nyuma ya raia na kwenye mahandaki kama wanavyofanya makamanda na viongozi wa Israel.  

Kwa upande mwingine, Hamas imesema kuwa shambulio la utawala huo kwenye Hospitali ya Ulaya huko Khan Yunis, kusini mwa Ghaza ni uhalifu na ni jinai mpya ya kivita ya Wazayuni.