Israeli yaua mwandishi mwingine wa habari Mpalestina
Jeshi la Israel lilimshambulia kwa risasi mwandishi wa habari Mpalestina katika eneo la kusini la Gaza, masaa machache baada ya yeye mwenyewe kutoa heshima kwa wenzake watano waliouawa katika mashambulizi ya awali ya Israel.
Hassan Douhan, mwandishi wa habari na mtaalamu ambaye alifanya kazi kama mwandishi kwa gazeti la al-Hayat al-Jadida, aliuawa kwa risasi za jeshi la Israel katika eneo la Khan Younis Jumatatu.
Kifo chake kinaongeza idadi ya waandishi wa habari waliouawa Gaza Jumatatu kuwa sita, na kuleta jumla ya wafanyakazi wa vyombo vya habari waliouawa tangu kuanza kwa vita vya mauaji ya kimbari vya Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza Oktoba 2023 kuwa 246.
Mapema, Israel ilitekeleza shambulio kwenye Kitio cha Matibabu cha Nasser huko Khan Younis, na kuua watu wasiopungua 20, wakiwemo waandishi watano wa habari na mhudumu wa afya, na kujeruhi wengine wengi.
Katika posti yake ya mwisho kwenye Facebook, Douhan alitoa heshima zake kwa waandishi watano waliouawa katika Hospitali ya Nasser.
“Mashahidi wa haki na kueneza ukweli…,” aliandika kuhusu waandishi wa habari waliouawa.
Kamati ya Kimataifa ya Kulinda Waandishi wa Habari (CPJ) imelaani shambulio hilo la kinyama la utawala wa Israel kwenye Hospitali ya Nasser, ikisisitiza kuwa jamii ya kimataifa inapaswa kuiwajibisha Israel kwa "mashambulizi yake dhidi ya vyombo vya habari."
Mkurugenzi wa CPJ wa Kanda, Sara Qudah, amesema kuuawa kwa waandishi wa habari na Israel katika Ukanda wa Gaza kunaendelea huku "dunia ikishuhudia na kushindwa kuchukua hatua kwa mashambulizi mabaya zaidi ambayo vyombo vya habari vimewahi kukumbana nayo katika historia ya hivi karibuni."
CPJ awali ilisema kuwa vita vya Israel dhidi ya Gaza vimekuwa vita vyenye madhara zaidi kwa waandishi wa habari vilivyorekodiwa.
Israel ilianzisha vita vya kimbari dhidi ya Gaza tangu Oktoba 7, 2023, baada ya wapiganaji wa Muqawama wa Hamas kufanya operesheni ya kushtukiza ya Kimbunga cha Al-Aqsa dhidi ya utawala wa Kizayuni kama jibu kwa kampeni ya miongo kadhaa ya utawala wa Israel ya jinai dhidi ya Wapalestina.
Mashambulizi ya kinyama ya utawala wa Israel dhidi ya Gaza hadi sasa yamesababisha vifo vya Wapalestina 62,800, wengi wao wakiwa wanawake na watoto.