Ripoti: Wayahudi huwatemea mate watalii Wakristo wanaotembelea Quds (Jerusalem)
-
Wayahudi huwatemea mate watalii Wakristo huko Quds
Ripoti mpya imeibua taswira ya matukio ya unyanyasaji na mashambulizi unaotekelezwa na Wayahudi dhidi ya wageni Wakristo wanaotembelea Mji wa Kale wa al-Quds (Jerusalem).
Hayo yanaripotiwa wakati watalii wa kimataifa wakianza kurejea katika maeneo yanayokaliwa na utawala wa Kizayuni wa Israel baada ya miaka miwili ya vita vya kikatili vya utawala huo dhidi ya Gaza vilivyoacha eneo hilo likiwa na njaa na maangamizi.
Kwa mujibu wa gazeti la Kiyahudi Israel Hayom, kumekuwa na taarifa za Wayahudi wa dhehebu la ultra-Orthodox wakitemea mate makundi ya Wakristo, hata mbele ya waongoza watalii wa ndani, katika wiki za karibuni.
Huduma ya simu ya dharura imerekodi matukio kadhaa ambapo wageni walitemewa mate walipokuwa wakipita katika mitaa ya Mji wa Kale, ikiwemo njia ya ibada ya Via Dolorosa. Ripoti hiyo imetaja visa vya vijana Wayahudi wakitemea mate Wakristo katika Njia ya Maumivu na tukio la kijana aliyeendesha baiskeli kumpiga teke mtalii huku akito vitisho.
Ripoti imeeleza kuwa mfumo wa elimu wa utawala wa Israel na mitazamo ya kijamii huchangia kukuza ujinga kuhusu Ukristo. Aidha dhana potovu ya ubora wa Wayahudi imekuwa chanzo cha kuchochea mashambulizi haya.
Halikadhalika imebainika kuwa mara nyingi mamlaka za Kizayuni hushindwa kulaani au kuchukua hatua za kuzuia unyanyasaji huo, na hivyo kuwaacha wageni bila ulinzi, kiasi cha baadhi yao kuficha alama za Kikristo haswa msalaba.
Mwezi uliopita, shirika la moja la Israel linalofuatilia mashambulizi dhidi ya Wakristo liliripoti kuwa karibu nusu ya mashambulizi katika Mji wa Kale wa al-Quds yalilenga Wakristo wa Kiarmeani.
Kituo cha Takwimu za Uhuru wa Kidini (RFDC), katika ripoti yake ya robo mwaka yenye kichwa Matukio Dhidi ya Wakristo Israel, kilirekodi jumla ya makosa ya chuki 31 dhidi ya Wakristo katika maeneo yaliyokaliwa kwa mabavu.
Ripoti hiyo, inayohusu kipindi cha Julai hadi Septemba 2025, ilibainisha kuwa asilimia 43 ya matukio yote katika Mji wa Kale wa al-Quds yalilenga Wakristo wa Kiarmeni.
Mashambulizi hayo yalihusisha kutemea mate, matusi ya maneno, uvamizi, uharibifu wa alama za kikrsito, uchafuzi, uchochezi mtandaoni, na udhalilishaji wa maeneo matakatifu, hasa ndani na kuzunguka Mji wa Kale wa al-Quds.