Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan baada ya uchaguzi wa Israel na ushindi wa vyama vya mrengo wa kulia
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i90274-ukingo_wa_magharibi_wa_mto_jordan_baada_ya_uchaguzi_wa_israel_na_ushindi_wa_vyama_vya_mrengo_wa_kulia
Usiku wa kuamkia Jumatatu vikosi vya utawala vamizi wa Israel vilishambulia maeneo mbalimbali ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Quds inayokaliwa kwa mabavu na kuwatia mbaroni vijana 20 wa Kipalestina.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Nov 09, 2022 02:47 UTC
  • Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan baada ya uchaguzi wa Israel na ushindi wa vyama vya mrengo wa kulia

Usiku wa kuamkia Jumatatu vikosi vya utawala vamizi wa Israel vilishambulia maeneo mbalimbali ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Quds inayokaliwa kwa mabavu na kuwatia mbaroni vijana 20 wa Kipalestina.

Lengo la kamatakama hii ni kuwazuia Wapalestina hao wasishiriki katika operesheni za utumiaji silaha na muqawama dhidii ya wanajeshi wa Israel. Ni kutokana na sababu hiyo ndio maana tangu miezi kadhaa iliyopita utawala haramu wa Iisrael umechukua hatua ya kupanua magereza yake. Hata hivyo utendaji huu wa Israel utashindwa na kugonga mwamba kutokana na sababu kadhaa.

Sababu ya kwanza ni kuwa, kutokana na eneo la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan kuungana na mhimili wa Jenin, Quds na kambi za wakimbizi wa Kipalestina huko Jordan, limeondokea kuwa na nafasi muhimu na maalumu na takribani Waarabu milioni 7 hadi 8 wa Kipalestina wanaishi katika maeneo na uwezekano wa kuwatia mbaroni wote ni jambo lisilowezekana.

Sababu ya pili ni kuwa, muqawama na mapambano ya Wapalestina hata baada ya kamatakamata ya Israel yangali yanaendelea na katika fremu hiyo, vikosi vya ukandamizaji vya utawala ghasibu wa Israel sambamba na kushambulia baadhi ya maeneo katika gereza la Hadarim, limefanya vitendo vya ukandamizaji dhidi ya mateka na wafungwa. Aidha wanajeshi hao wamefanya upekuzi mkali katika vyumba vya mateka hao na kusambaratisha vitu na vifaa vyao binafsi.

Nukta ya tatu ni kuwa, utawala bandia wa Israel sanjari na kutekeleza operesheni kubwa ya kamakata na utiaji mbaroni ulio kinyume cha sheria umekuwa ukikiuka wazi na bayana kabisa mikataba ya kimataifa na hivyo kulifanya faili lake la jinai za kivita kuwa zito na kubwa zaidi.

 

Takwimu zinazotolewa na duru za Kipalestina zinaonyesha kuwa, kuna takribani mateka 4,500 wa Kipalestina katika magereza ya Israel wakiwemo wanawake 131 na watoto 175. Aidha mateka zaidi ya 700 miongoni mwao wamo katika magereza hayo wakiwa wanashikiliwa kwa muda.

Tangu ulipoanza mwaka huu hadi sasa utawala wa Kizayuni wa Israel umepasisha hukumu 1800 za kushikiliwa kwa muda Wapalestina. Kushikiliwa kwa muda ni sheria inayotekelezwa na Israel ambapo katika kipindi hicho, mtuhumiwa hushikiliwa bila ya kushtakiwa wala kesi yake kusikiiliwa kama ambavyo katika muda huo hana ruhuua ya kukutana na wakili, hatua ambayo inakinzana waziwazi na haki za binadamu za kimataifa. Mbinu hii duniani imekuwa ikitekelezwa na Israel pekee.

Sababu ya nne ni kuwa, kadiri wanajeshi wa utawala haramu wa Israel watakavyofanya hujuma zenye wigo mpana katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan kwa ajili ya kuwatia mbaroni Wapalestina ndivyo pia vikosi vya muqawama na mapambano vya Kipalestina vinavyojipanga na kuimarisha mbinu zake za kujihami na kukabiliana na mashambulio na jeshi la Wazayuni maghasibu. Idhaa ya jeshi la utawala bandia wa Israel imekiri bayana katika matangazo yake kwamba, katika mwezi uliopita wa Oktoba Wapalestina wametekeleza operesheni 382 dhidi ya wanajeshi wa Israel na walowezi wa Kizayuni kama mashambulio ya visu, mawe, mabomu ya mkono na kadhalika ambapo ikilinganishwa na mwezi Septemba ambapo kulisajiliwa matukio 254 kuna ongezeko na mashambulio 130.

Benjamin Netanyahu

 

Sababu ya tatu ni kuwa, filihali Wapalestina wamefikia welewa na ufahamu huu kwamba, umoja baina ya makundi na mirengo yote ya kisiasa ya Palestina ndio silaha muhimu kabisa ya kistratejia kwa ajili ya kukabiliana na siasa za kujitanua za Israel katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na njama za kutaka kukamilisha mpango wa kuuyahudisha mji wa Quds na kubomoa msikiti wa al-Aqswa.

Baada ya kikao cha Algeria cha makundi ya Kipalestina kumejitokeza matumaini mapya Palestina hasa baada ya kufikiwa maridhiano ya kitaifa, kuendeleza msingi wa ushirikishaji wa kisiasa utakaojumuisha pande zote na vyama mbalimbali vya kitaifa vya Palestina kupitia uchaguzi, na kuchukuliwa hatua za haraka kwa ajili ya kuitisha uchaguzi wa kitaifa katika maeneo yote ya Palestina kwa mujibu wa sheria zilizopitishwa.

Hivi sasa tumaini na tegemeo pekee la Wazayunii wenye kufurutu mpaka ni kurejea tena Benjamin Netanyahu katika ulingo wa siasa za Israel. Hata hivyo tumaini hilo nalo ni ndoto za alinacha. Hii ni kutokana na kuwa, kwanza Netanyahu hana dawa mujarabu ya kutibu matatizo ya sasa ya utawala huo ghasibu. Pili ni kuwa, mwenyewe anakabiliwa na mlolongo wa mafaili ya ufisadi, mafaili ambayo hadi sasa yapo wazi.

Tatu ni kwamba, kurejea Netanyahu katika hatamu za uongozi wa Israel kuna hatari ya kutengwa utawala huo hasa kwa kutilia maanani kwamba, hata sasa ukimuondoa Rais Volodymyr Zelenskyy wa Ukraine hadi sasa hakuna kiongozi mwingine wa dunia aliyempongeza Netanyahu baada ya kupata ushindi katika uchaguzi wa Bunge hivi karibuni.

Jambo la nne ni kuwa, ushindi wa chama cha Likud kabla ya kuzungumzia kwamba, umetokana na kupendwa chama hicho, zaidi umetokana na kudhoofika kambi hasimu. Nukta ya tano ni kwamba, uchaguzi wa hivi karibuni wa Bunge la Israel pamoja na matokeo yake haujabadilisha kitu katika jamii pinzani ya Israel badala yake umeidondosha tu serikali ya Waziri Mkuu Yair Lapid na nafasi yake kuchukuliwa na muungano wa Netanyahu huku asili ya mizozo na mivutano pamoja na sababu zake zikiendelea kubakia vilevile.