Kuendelea kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu barani Ulaya
Vitendo vya kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu vinaendelea kushuhudiwa barani Ulaya chini ya kivuli cha uhuru wa kusema au wa kutoa maoni.
Licha ya radiamali kubwa ya Waislamu na mataifa ya Kiislamu dhidi ya kitendo cha kuchomwa moto Qur'ani Tukufu katika mataifa mawili ya Ulaya Mashariki yaani Sweden na Denmak na upinzani wa wazi wa Umoja wa Mataifa kwa kitendo hicho na hata kutolewa matamshi na viongozi wa mataifa hayo mawili ya kuzuia vitendo kama hivyo, lakini kwa mara nyingine tena watu wenye chuki na Uislamu wamekivunjia heshima Kitabu kitakatifu cha Qur'ani. Kwa mara ya tatu polisi ya Sweden imetoa kibali kwa Salwan Momika raia wa nchi hiyo kufanya mkusanyiko mbele ya Bunge na kuchoma moto nakala ya Qur'ani.
Video iliyosambaa katika mitandao mbalimbali inamuonyesha mtu huyo mwenye chuki dhidi ya Uislamu akiwa pamoja na mwenzake wakivunjia heshima Qur'ani Tukufu mbele ya Bunge la Sweden. Salwan Momika na Salwan Najm baada ya kuvunjia heshima Qur'ani walichoma moto kurasa zake mbele ya hadhirina. Salwan Najm ambaye kabla ya hapo alishirikiana na Momika katika matukio mawili ya hivi karibuni ya kuvunjia heshima Qur'ani Tukufu amesema kuwa: Tutaendelea na kitendo hiki mpaka pale Qur'ani itakapopigwa marufuku nchini Sweden. Sambamba na tukiio hilo, watu wenye misimamo mikali wa mrengo wa kulia huko nchini Denmark kwa mara nyingine tena wamechoma moto Qur'ani Tukufu katika mji mkuu wa nchi hiyo Copenhagen.
Uhusiano wa Sweden na mataifa ya Kiislamu umeharibika katika majuma ya hivi karibuni kufuatia matukio ya kuvunjiwa heshima Qur'ani katika taifa hilo. Serikali ya Iraq imechukua hatua kubwa zaidi miongoni mwa mataifa ya Kiislamu baada ya kumuita nyumbani balozi wake nchini Sweden na kumtimua nchini humo balozi wa taifa hilo la Ulaya.
Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) Jumatatu ya juzi iliitisha kikao cha dharura ambapo ililaani vikali vitendo vya kuvunjiwa heshima Qur'ani katika mataifa mawili ya Swden na Denmark. Taarifa iliyotolewa mwishoni mwa kikao hicho ilieleza: Tunasikitishwa sana na kukaririwa vitendo vya kuvunjia heshima Qur'ani Tukufu na kuendelea kutolewa vibali na viongozi wa Sweden vya kuidhinisha vitendo kama hivi na kutochukuliwa hatua za kuzuia kukaririwa vitendo kama hivi huko Sweden na Denmark. Sehemu nyingine ya taarifa hiyo inaeleza kuwa, upuuzaji wa viongozi wa Denmark na Sweden na kutochukua hatua za kuzuia kuvunjiwa heshima Qur'an kunakinzana wazi na azimio nambari 2686 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa la 14 Juni mwaka huu (2023) kuhusiana na amani na usalama wa kimataifa.
Licha ya radiamali kali za Waislamu, mataifa ya Kiislamu na hata Umoja wa Mataifa dhidi ya mamluki wa Uzayuni kama Momika Salwan ambaye mfungamano wake na Tel Aviv ni jambo lisilo na shaka, lakini mataifa ya Magharibi yangali yanatoa idhini kwa watu wenye chuki na Uislamu kuvunjia heshima matukufu ya Kiislamu hususan kuchomwa moto Qur'ani Tukufu.
Himaya na uungaji mkono wa Wamagharibi kwa kitendo cha kuvunjiwa heshima na cha kuchomwa moto Qur'ani unafanyika katika hali ambayo, Umoja wa Mataifa unapinga kitendo hicho cha aibu. Farhan Haq, Naibu msemaji wa Umoja wa Mataifa anasema: Miguel Moratinos, Mkuu wa Asasi ya Staarabu ya Umoja wa Mataifa amelaani vikali kuchomwa moto Qur'ani Tukufu mbele ya msikiti mmoja katikati ya mji wa Stockholm, Sweden.
Inaonekana kuwa, Wamagharibi wanapuuza kwa makusudi tofauti baina ya uhuru wa kusema na kutusi matukufu ya dini. Tukitupia jicho vigezo vya kindumakuwili vya madola Magharibi zikiwemo Sweden na Denmark kuhusiana na uhuru wa kutoa maoni tunaona kuwa, jambo hili hubeba maana pale tu linapohoji na kuvunjia heshhima jambo ambalo ndio mtazamo wa Magharibi kama vile chuki dhidi ya Uislamu na kuvunjia heshima matukufu ya Waislamu. Lakini mambo ni kinyume kabisa kuhusiana na masuala mengine kama ngano ya Holocaust. Mfano mwingine wa wazi ni vita vya Ukraine na Russia ambapo wanaotoa maoni na mitazamo kuhusu vita hivyo ambayo ni kinyume na matazmo wa madola ya Magharibi hukabuiliwa na mashinikizo ya kila upande na wakati mwingine kukabiliwa na mashtaka kama ilivyo katika suala la Holocaust.