Tarehe 21 Agosti; Siku ya Kimataifa ya Misikiti.
https://parstoday.ir/sw/news/world-i101360-tarehe_21_agosti_siku_ya_kimataifa_ya_misikiti.
Sababu iliyopelekea siku hii kutengwa kama Siku ya Kimataifa ya Misikiti inahusiana na tukio lililotokea miaka 56 iliyopita katika Msikiti Mtukufu wa Al-Aqsa, katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na utawala ghasibu wa Israel, na ambao ni Kibla cha kwanza cha Waislamu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 22, 2023 09:01 UTC
  • Tarehe 21 Agosti; Siku ya Kimataifa ya Misikiti.

Sababu iliyopelekea siku hii kutengwa kama Siku ya Kimataifa ya Misikiti inahusiana na tukio lililotokea miaka 56 iliyopita katika Msikiti Mtukufu wa Al-Aqsa, katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na utawala ghasibu wa Israel, na ambao ni Kibla cha kwanza cha Waislamu.

Saa moja asubuhi tarehe 21 Agosti 1969, Mzayuni mwenye itikadi kali kwa jina Dennis Michael William Rohan aliuchoma moto Msikiti wa Al-Aqsa kwa msingi wa hatua iliyopangwa vyema na kuungwa mkono na serikali ya wakati huo ya utawala haramu wa Israel. Kutokana na kitendo hicho cha kinyama na chuki za kidini, mitamraba 1,500 za eneo la msikiti huo ziliteketezwa.

Kufuatia kitendo hicho cha jinai, Msikiti wa Omar, Mihrabu ya Zakariya, Maqam ya Arbaeen, kumbi tatu za msikiti huo pamoja na nguzo zinazobeba kuba la Msikiti wa al-Aqsa vilichomeka kwenye moto huo, na paa la msikiti kuporomoka.

Baada ya moto huo kuzimwa, utawala wa Kizayuni ulihusisha kitendo cha uteketezaji wa Msikiti wa al-Aqsa na mtalii mmoja wa Australia na baada ya kumtia mbaroni mtalii huyo wa Kizayuni na kuanzisha kesi ya kimaonyesho tu dhidi yake huko Tel Aviv, utawala huo ulimtangaza kuwa mgonjwa wa akili na hivyo kumwachia huru.

Tangu kukamilika ukaliwaji wa mabavu wa Palestina katika vita vya siku 6 vya mwaka 1967 vilivyoteka pia maeneo ya mashariki mwa Jerusalem, watawala wa Kizayuni wamekuwa wakitekeleza mipango na njama za kuuharibu kabisa Msikiti wa al-Aqsa. Madhumuni ya uharibifu huo ni kuweka mahala pake msingi wa ujenzi wa hekalu bandia eti la Nabii Suleiman (as), jambo ambalo bado linafuatiliwa kwa nguvu zote na Wazayuni wenye misimamo mikali, na hasa katika kipindi hiki cha utawala wenye itikadi kali wa Benjamini Netanyahu.

Msikiti Mtukufu wa al-Aqsa

Uchomaji wa msikiti huo mtakatifu ulizua lawama na ukosoaji mkali wa kimataifa. Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilikutana na kupitisha azimio nambari 271 mwaka 1969, ambalo liliulaani utawala haramu wa Israel kuhusiana na kitendo hicho.

Waislamu katika pembe mbalimbali za dunia na bila kujali propaganda zilizoenezwa na utawala huo unaoikalia kwa mabavu Quds Tukufu na waungaji mkono wake wa Magharibi, walifanya maandamano makubwa kupinga hatua hiyo ya utawala wa Kizayuni. Serikali za Kiislamu pia zilichukua hatua na kuunda "Jumuiya ya Nchi za Kiislamu" ili kukabiliana na hatari zinazotishia ulimwengu wa Kiislamu na matukufu yake.

Msikiti wa al-Aqsa unachukuliwa kuwa na utukufu wa hali ya juu katika Uislamu, na ni wa tatu kwa umuhimu baada ya Masjid al-Haram na Masjid al-Nabii. Kwa mujibu wa Riwaya, Mtume Muhammad (saw) alipanda kwenda mbinguni kutokea hapo, katika tukio la kihistoria linalojulikana kama Mi'raj, na ambalo limetajwa katika Surat al Israa katika kitabu kitakatifu cha Qur'ani.

Utawala wa Kizayuni kama tulivyotangulia kusema umekuwa ukifuatilia mipango ya kuuharibu kabisa Msikiti wa al-Aqsa ikiwa ni katika malengo ya kistratijia ya utawala huo, na unatumia kila fursa inayojitokeza kuuharibu kabisa, ambapo siasa hizo haribifu na za jinai zimepata msukumo na kasi kubwa hasa baada ya kuundwa serikali ya Netanyahu yenye misimamo mikali ya kupindukia mipaka. Pamoja na hayo lakini mwamko, nguvu ya mapambano na kuwa macho watu wa Palestina kumezuia pakubwa utekelezwaji wa vitisho vinavyohatarisha msikiti huo mtukufu.

Kwa upande mwingine, Siku ya Msikiti Duniani ni fursa nyingine ambayo inawapa watu nafasi ya kuzingatia hadhi ya msikiti katika hali yake ya kisasa. Kila dini ina alama na nembo zake maalumu ambapo Uislamu ambao ni dini ya mwisho ya mbinguni, umeipa umuhimu mkubwa nafasi ya msikiti na kanuni zake miongoni mwa wafuasi wake.

Masjid al-Haram mjini Makka

Msikiti sio tu ni mahali pa kuabudu na kumuomba Mwenyezi Mungu, bali pia ni sehemu ya kujadili na kubadilishana mawazo kuhusu masuala ya kiuchumi, kijamii, kisiasa na kijeshi. Kwa hakika, msikiti ni mahala pa kufanyika mashauriano na kuchukuliwa maamuzi ya Waislamu, ushirikiano katika mambo yanayopaswa kutekelezwa, sehemu ya kukusanyika na kukutana Waislamu kwa ajili ya kuonyesha umoja na mshikamano wao, kituo cha  mafunzo ya msingi ya kijeshi kwa ajili ya kulinda nchi, mahala pa kufunza na kujifundisha na vilevile kutatua masuala ya kidini na yanayoibua shaka na mahala pa kuchanganya na kuunganisha dini na siasa. Kwa ufupi ni kwamba msikiti una kazi nyingi na zenye malengo tofauti ya kuhudumia dini na maslahi ya Waislamu.

Tangu mwanzo wa kuasisiwa kwake hadi leo, msikiti umekuwa kituo muhimu cha kufikisha na kutekeleza ujumbe wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw), chanzo cha maendeleo, huduma na msingi wa kufikisha ujumbe wa Mwenyezi Mungu. Hivi sasa pia, msikiti unatumika kendeshea shughuli tofautii katika nyanja mbalimbali, na kadiri shughuli hizo zinavyokuwa tofauti, ndivyo zinavyovutia na kupokelewa zaidi na matabaka yote ya jamii na hasa kizazi cha vijana. Matokeo yake bila shaka ni kuongezeka imani na itikadi za kidini, kutumika wakati katika mazingira bora na salama kabisa ya Kiislamu na kidini, kupatikana uchangamfu na ushiriki wa kijamii pamoja na faida nyingine nyingi katika ngazi ya jamii.