Kufukuzwa makumi ya wanadiplomasia wa Canada nchini India
https://parstoday.ir/sw/news/world-i103064-kufukuzwa_makumi_ya_wanadiplomasia_wa_canada_nchini_india
Siku ya Jumanne, serikali ya India iliitaka serikali ya Canada kuwaondoa wanadiplomasia wake wengine 40 kutoka nchi hiyo. Takwa hilo la kufukuzwa idadi kubwa ya wanadiplomasia wa Canada linaonyesha kuongezeka mvutano katika uhusiano wa nchi mbili.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 04, 2023 22:50 UTC
  • Kufukuzwa makumi ya wanadiplomasia wa Canada nchini India

Siku ya Jumanne, serikali ya India iliitaka serikali ya Canada kuwaondoa wanadiplomasia wake wengine 40 kutoka nchi hiyo. Takwa hilo la kufukuzwa idadi kubwa ya wanadiplomasia wa Canada linaonyesha kuongezeka mvutano katika uhusiano wa nchi mbili.

Mvutano katika uhusiano wa pande mbili hizo ulianza kudhihiri kufuatia kuuawa karibuni nchini Canada kiongozi wa Makalasinga wanaotaka kujitenga nchini India ambapo serikali ya Canada iliinyooshea kidole cha lawama serikali ya New Delhi. Serikali ya Canada ilimfukuza mwanadiplomasia wa India kufuatia tuhuma hizo, nayo India ikachukua hatua ya kulipiza kisasi. Katika hatua ya pili India imetaka kufukuzwa nchini humo wanadiplomasia 40 wa Canada jambo linaloonyesha wazi kuwa mvutano katika uhusiano wa pande hizo sio tu haujapungua bali unaendelea kuongezeka.

Soroush Amiri, mtaalamu wa masuala ya India, anasema kuhusu jambo hili kwamba India inajaribu kukabiliana na Canada kama nchi kubwa na muhimu duniani. Ingawa muhusika wa mauaji ya kiongozi wa Masingasinga wanaotaka kujitenga nchini Canada hajatambuliwa, lakini kwa kukabiliana vikali na Canada, India inataka kuonyesha kuwa New Delhi haitakubali kutuhumiwa na nchi za Magharibi, ili nchi kama Canada, ambayo inachukuliwa kuwa chini ya udhibiti wa Uingereza, isithubutu kutoa tuhuma zisizo na msingi dhidi yake.

Tishio la India kwamba iwapo Canada haitawaondoa wanadiplomasia wake kutoka nchi hiyo kufikia tarehe 10 Oktoba, haitadhamini tena kinga yao ya kidiploamsia, ni maneno ya kuonyesha nguvu ya New Delhi ili Ottawa ikomeshe uingiliaji wake katika masuala ya ndani ya India. Inaonekana kwamba serikali ya India, kwa kuongeza mashinikizo ya kisiasa dhidi ya Canada, inajaribu kuilazimisha nchi hiyo iwafukuze nchini humo Masingasinga wanaotaka kujitenga na wapinzani wengine wa serikali ya India.

Mvutano katika uhusiano wa India na Canada

Kwa mtazamo wa India, mvutano wa sasa na Canada umetoa fursa nzuri kwa ajili ya New Delhi kutoa mashinikizo ya kidiplomasia kwa Ottawa ili ilazimike kuwafukuza Masingasinga hao na wapinzani wengine wa serikali ya India. Inasema nchi za Magharibi zimekuwa wafadhili na maficho ya wapinzani, magaidi na wanaotaka kujitenga katika nchi tofauti ili kuwatumia kama chombo cha kutoa mashinikizo kwa nchi kama India.

AM Ram Singh, mtaalamu wa masuala ya kisiasa, anasema, kwa kukabiliana vilivyo na Canada, serikali ya India inataka kutuma ujumbe huu kwa nchi nyingine za Magharibi kwamba zikomeshe mwenendo wa kulea wapinzani wa nchi na serikali tofauti kwa ajili ya kuwatumia kama chombo cha kutolea mashinikizo dhidi ya serikali hizo.

Kwa vyovyote vile, matarajio ya nchi kama India kwa Canada ni kuheshimu uhuru na kujitawala mataifa, kwa sababu nchi zenye kiburi za Magharibi huhifadhi na kuwalea wapinzani wa nchi tofauti, na hii ni katika hali ambayo kipindi cha uingiliaji kama huo kimepitwa na wakati. Nchi kama India zimeonyesha kivitendo kuwa hazitaruhusu nchi za Magharibi kuingilia masuala yao ya ndani kupitia makundi ya kigaidi.

Kwa sababu hiyo, serikali ya India imepuuzilia mbali matamshi yaliyotolewa na viongozi wa Canada, akiwemo Waziri Mkuu wa nchi hiyo, juu ya kuhusika New Delhi katika mauaji ya kiongozi wa Masingasinga anayeitwa Hardeep Singh Najjar, na kumtangaza kuwa gaidi kutokana na fikra zake za kujitenga. Nukta nyingine muhimu katika vita vya kidiplomasia kati ya India na Canada ni kwamba kwa mtazamo wa India, idadi na vyeo vya wanadiplomasia wa kila nchi katika ardhi ya upande wa pili vinapaswa kuwa sawa na inaonekana kuwa kufukuzwa wanadiplomasia wa Canada huko India kunalenga kusawazisha idadi ya wanadiplomasia wake na wa Canada.