Human Rights Watch yatoa wito wa kushughulikiwa hatari za roboti wauaji
(last modified Tue, 29 Apr 2025 02:43:51 GMT )
Apr 29, 2025 02:43 UTC
  • Human Rights Watch yatoa wito wa kushughulikiwa hatari za roboti wauaji

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limetahadharisha kuhusu hatari kubwa ya silaha zinazojiendesha zenyewe kwa haki za binadamu wakati wa vita na amani.

Shirika hilo limetoa wito kwa serikali za nchi mbalimbali kushughulikia wasiwasi ulioibuliwa na silaha hizo zinazojulikana kama "roboti wauaji," (killer robots) kwa kujadili mkataba wa kimataifa wa kushughulikia hatari hizo, kabla ya mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuhusu silaha hizo huko New York katikati ya Mei 2025.

Ripoti iliyotolewa na shirika hilo imeangazia mgongano kati ya silaha hizo na haki za kimsingi za binadamu, kama vile haki ya kuishi, kufanya mikusanyiko ya amani, faragha, haki ya kupata suluhisho la madhara yanayotokea kwa mtu baada ya kushambuliwa, pamoja na kanuni zinazohusiana na utu na kutobaguliwa.

Human Rights Watch imeeleza kuwa "matumizi ya silaha zinazojiendesha zenyewe hayataishia kwenye vita tu, bali yataenea hadi kwenye operesheni za utekelezaji wa sheria, udhibiti wa mipaka na hali nyinginezo, jambo linaloibua wasiwasi mkubwa chini ya sheria za kimataifa za haki za binadamu."

"Ili kuepuka mustakabali wa mauaji ya kiotomatiki, serikali zinapaswa kutumia kila fursa kufikia mkataba wa kimataifa kuhusu silaha zinazojiendesha," imeongeza taarifa ya Human Rights Watch.

Silaha zinazojiendesha zenyewe hufanya kazi kulingana na programu ambayo inategemea algoriti na maingizo kutoka kwa vitambuzi vingi kama vile kamera, sahihi za rada na data ya joto.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, silaha hizi hazina uwezo wa kutafsiri hali ngumu au uamuzi na hisia za kibinadamu ambavyo ni vipengele muhimu kwa ajili ya kuhakikisha utekeleza wa sheria za kimataifa na kuhakikisha matumizi ya chini ya nguvu.