Mawakili wa Uingereza katika vita vya kisheria dhidi ya Uzayuni
Dunia imeshuhudia karibu miezi 23 ya mauaji ya wazi dhidi ya watu wa Palestina yanayofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel.
Kampeni hii ya umwagaji damu imepelekea zaidi ya Wapalestina 62,800 wa Gaza kuuawa, huku takriban watu 380,000 wakitoweka na kuna uwezekano mkubwa kuwa wamepoteza maisha.Kwa jumla, inakadiriwa kuwa takriban watu 450,000 wa Gaza wamepoteza maisha tangu tarehe 7 Oktoba 2023 na wengi wao ni wanawake na watoto.
Kwa sababu ya ghadhabu kubwa iliyoibuka kutokana na unyama huu, ushawishi wa Kizayuni nchini Uingereza umechukua hatua za kujaribu kunyamazisha harakati za kuunga mkono Palestina kwa vitisho vya kisheria, wakilenga hasa waandaaji maandamano na wale wanaothubutu kusema hadharani.
Harakati za Kizayuni nchini Uingereza, zikiongozwa na makundi kama UK Lawyers for Israel, zimekuwa mstari wa mbele kutumia vitisho vya kisheria kunyamazisha watu. Mbinu zao zimejumuisha vitisho vya mashitaka na pia kushinikiza sehemu zinazowakaribisha wanaharakati wa Palestina zifunge milango yao.
Hata hivyo, kundi la wanasheria wenye weledi limeamua kutosalia kimya. Mradi mpya uitwao Riverway to the Sea umeanzishwa ili kutoa elimu ya kisheria na kuwapatia wanasheria, wanaharakati na jamii zana za kupinga Kizayuni. Mradi huu umeanzishwa na mawakili mashuhuri wa Uingereza, Fahad Ansari na Frank McGuinness, ambao wamelikabili moja kwa moja shinikizo la Kizayuni.
Fahad Ansari anasema ni muhimu watu wafahamu kuwa Wazayuni hawana uhalali wa kimaadili. Mara kwa mara hujaribu kudai nafasi hiyo ya maadili ili kukufanya ujisikie vibaya unaposhikamana na waliodhulumiwa. Lakini ukweli ni kwamba, sisi ndio tuna uhalali wa kimaadili, na hatupaswi kuusahau. Vitisho, mbinu za mabavu, na kampeni za matusi havina tena nguvu.
Moja ya silaha kuu zinazotumiwa na Wazayuni ni kundi UK Lawyers for Israel, linaloungwa mkono na watu wenye nguvu na utajiri miongoni mwa Wayahudi, ili kuwatisha wale wanaounga mkono Palestina. Lakini kundi hilo sasa limewekwa chini ya uchunguzi na mdhibiti wa mashirika ya hisani nchini Uingereza, kufuatia malalamiko ya kisheria kutoka kwa wanaharakati, jambo linaloonyesha mipaka ya nguvu za Kizayuni hata katika nchi za Magharibi.
Licha ya propaganda kuegemea upande wa utawala wa Kizayuni na wafuasi wake nchini Uingereza, wanasheria hawa na wengine zaidi wamekataa kuogopeshwa.
Wanaendelea kupigana kwa kutumia kila nyenzo waliyonayo, wakiwa bega kwa bega na wananchi wa Palestina wanaoendelea kukabiliwa na dhulma na mauaji ya kimbari yanayotekelezwa na utawala dhalimu wa Israel