Azma ya Malaysia ya uungaji mkono endelevu kwa Palestina
https://parstoday.ir/sw/news/world-i130086-azma_ya_malaysia_ya_uungaji_mkono_endelevu_kwa_palestina
Naibu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Malaysia amesema kuwa, nchi hiyo itadhibiti na kusimamia vilivyo vitisho au ugaidi wowote unaohusiana na suala la uungaji mkono wa Kuala Lumpur kwa Palestina na kuwa itadumisha misimamo ya kuwaunga mkono Wapalestina dhidi ya utawala wa Kizayuni.
(last modified 2025-08-28T04:17:54+00:00 )
Aug 28, 2025 04:17 UTC
  • Azma ya Malaysia ya uungaji mkono endelevu kwa Palestina

Naibu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Malaysia amesema kuwa, nchi hiyo itadhibiti na kusimamia vilivyo vitisho au ugaidi wowote unaohusiana na suala la uungaji mkono wa Kuala Lumpur kwa Palestina na kuwa itadumisha misimamo ya kuwaunga mkono Wapalestina dhidi ya utawala wa Kizayuni.

Mohammad Alamin, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Malaysia ameongeza kuwa: "Msimamo wa nchi hii kuhusu Palestina umekuwa thabiti kwa miongo kadhaa na inawaunga mkono Wapalestina."

Amesema kwenye ukumbi wa Bunge la Malaysia kwamba: "Kuhusu vitisho au ugaidi unaoweza kufanywa dhidi yetu kwa kuunga mkono suala la Palestina, ninaamini hili ni jambo ambalo tunaweza kulidhibiti kwa sababu msimamo wetu katika suala hili ni imara."

Ameongeza kuwa: "Sera ya kigeni ya Malaysia katika Mashariki ya Kati inabakia kuwa ya kina, yenye misingi thabiti na ya kivitendo, ikisisitiza diplomasia na ushirikiano wa karibu na nchi kama vile Jordan, Misri, Türkiye na Qatar ili kutatua migogoro kwa amani."

Alisisitiza msaada mkubwa wa Malaysia kwa Palestia kwenye jukwaa mbalimbali za kimataifa ikiwemo Umoja wa Mataifa, Shirika la Ushirikiano wa Kiislamu (OIC), Harakati ya Kutokubaliana (NAM) na Jumuiya ya Mataifa ya Kusini-Mashariki mwa Asia (ASEAN).

Wakati huo huo,  Maelfu ya Wamalaysia, wakiongozwa na Waziri Mkuu Anwar Ibrahim Jumapili, walijaza Uwanja wa Merdeka maarufu huko Kuala Lumpur kuonyesha mshikamano na wananchi wa Gaza na kulaani vitendo vya Israel.

Wakiwa wamevaa nguo nyeupe na vilemba vya Kipalestina maarufu kama Keffiyeh, wanaume, wanawake na watoto walikusanyika kuonyesha mshikamano wao na Gaza huku Anwar akiahidi msaada zaidi kwa eneo lililoharibiwa na vita.

Tukio la jioni lililopewa jina la “Malaysia Yangu Na Gaza” lilikuwa kilele cha Tamasha la Sumud Nusantara la siku tatu lililofanyika kuanzia Agosti 22 hadi 24.

Maandamano hayo yaliandaliwa kwa pamoja na Baraza la Ushauri la Mashirika ya Kiislamu Malaysia (MAPIM) na Cinta Gaza Malaysia (CGM), huku likiungwa mkono na ofisi ya waziri mkuu.