Venezuela yashukuru Iran kwa mshikamano dhidi ya vitisho vya uvamizi vya Marekani
Waziri wa mambo ya nje wa Venezuela ameishukuru Iran kwa msimamo wake thabiti wa kuunga mkono taif hilo a la Amerika ya Kusini mbele ya vitisho vya uchokozi vinavyotolewa na Marekani.
Yván Eduardo Gil Pinto alitoa kauli hiyo katika mazungumzo ya simu na mwenzake wa Iran, Abbas Araghchi, ambapo mawaziri hao wawili walibadilishana mawazo kuhusu uhusiano wa Tehran na Caracas pamoja na matukio mapya katika ukanda wa Karibiani.
Katika mazungumzo hayo, waziri wa mambo ya nje wa Venezuela alimfahamisha Araghchi kuhusu kuongezeka kwa mvutano katika eneo la Karibiani kufuatia vitisho vya Marekani na madai yasiyo na msingi dhidi ya taifa la Amerika ya Kusini.
Akiishukuru Iran kwa mshikamano na msaada wake kwa Venezuela, Pinto alisisitiza dhamira ya wananchi na serikali ya Venezuela kulinda uhuru wa taifa na heshima ya mamlaka yake ya kitaifa mbele ya vitisho vya uvamizi kutoka Marekani.
Kwa upande wake, Araghchi alionya juu ya hatari inayoongezeka kutokana na msimamo wa Marekani wa kujitwalia maamuzi yenye sura ya mabavu, hali inayotishia amani na uthabiti wa dunia nzima.
Akiilaani hatua ya Marekani kuibebesha Venezuela tuhuma zisizo na msingi na tishio la kutumia nguvu dhidi ya Caracas, waziri wa mambo ya nje wa Iran alithibitisha tena mshikamano wa Jamhuri ya Kiislamu na Venezuela.
Venezuela tayari imetangaza kuwa imepeleka meli za kivita na ndege zisizo na rubani kwenye eneo lake la maji na kufanya doria kwenye ufuo wa pwani ya nchi hiyo ili kukabiliana na hatua ya Marekani ya kutuma meli kadhaa za kivita katika eneo la Karibiani kwa kile ilichodai ni kwa ajili ya kukabiliana na biashara ya madawa ya kulevya na kumshinikiza Rais Nicolás Maduro.
Waziri wa Ulinzi wa Venezuela, Vladimir Padrino, amesema katika video iliyowekwa kwenye mitandao ya kijamii kwamba "doria za majini zimetumwa kwenye Ghuba ya Venezuela na pwani ya Karibea, na meli kubwa kaskazini mwa eneo letu la maji," pamoja na "idadi kubwa ya ndege zisizo na rubani."