Jun 28, 2016 04:24 UTC
  • Jumanne, Juni 28, 2016

Leo ni Jumanne tarehe 22 Ramadhani mwaka 1437 Hijria sawa na Juni 28 mwaka 2016.

Miaka 1164 iliyopita katika siku kama hii ya leo, alifariki dunia Ibn Majah, mpokezi wa hadithi na mfasiri mashuhuri wa Qur’ani wa Kiislamu. Ibn Majah alizaliwa mwaka 209 Hijria katika mji wa Qazvin nchini Iran. Alielekea katika nchi mbalimbali za Kiislamu ili kujifunza elimu ya hadithi. Aliandika kitabu chake mashuhuri kwa jina la "Sunan Ibn Majah" baada ya kuhitimu masomo katika elimu ya hadithi, kitabu ambacho ni moja kati ya vitabu sita vya hadithi vyenye itibari vya Waislamu wa madhehebu ya Suni.

Miaka 143 iliyopita na katika siku kama ya leo alizaliwa Dakta Alexis Carrel mwanabiolojia na mwanafalsafa wa Kifaransa. Baba yake alikuwa mfanyabiashara na aliaga dunia na kumuacha akiwa angali kijana mdogo. Mwaka 1912 Dakta Carrel alitunukiwa tuzo ya heshima ya Nobeli kutokana na mchango wake mkubwa katika uwanja wa tiba. Mwanafalsafa huyo aliutambua utamaduni wa Kiislamu baada ya kusafiri na kuyatembelea maeneo kadhaa ya ardhi za Kiislamu. Kitabu mashuhuri mno cha Alexis Carrel ni :‘' "Man The Unknown''.

Siku kama ya leo miaka 10 iliyopita sawa na tarehe 28 mwezi Juni mwaka 2006 jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel lilianzisha mashambulio makubwa ya nchi kavu na angani huko katika Ukanda wa Ghaza. Utawala wa Kizayuni uliendesha mashambulio hayo ya kinyama kwa kisingizio cha kuuawa wanajeshi wake wawili na wanamuqawama wa Kipalestina siku tatu kabla ya mashambulio hayo. Utawala haramu wa Israel ulidai kuwa wanamapambano wa Palestina walifanya oparesheni katika kituo kimoja cha upekuzi na kupelekea kuuawa wanajeshi wake wawili na kukamatwa mateka mwingine mmoja. Idadi kadhaa ya mawaziri, wabunge na wawakilishi wa baraza la mji la serikali halali ya Palestina inayoongozwa na harakati ya Hamas walitekwa nyara na wanajeshi wa Israel katika siku za kwanza za mashambulizi hayo makubwa ya jeshi la utawala wa Kizayuni huko Ghaza yaliyopewa jina la "Mvua za Kiangazi". Mbali na hao, mamia ya raia madhlumu wa Palestina waliuawa shahidi na wengine kujeruhiwa katika mashambulizi ya kinyama ya anga na nchi kavu ya utawala wa Kizayuni dhidi ya Ukanda wa Ghaza.